SERIKALI INAWAJALI WANAWAKE NA WATOTO: Mhe, MWANAIDI

Na WMJJWM,Dar es salaam
Serikali inaendelea kutekeleza afua zinazolenga kuboresha afya na ustawi wa Watoto na Wanawake kupitia jitihada mbalimbali ambazo zinajumlisha kujenga na kukarabati Vituo vya Afya, kununua Vifaa Tiba,kuwajengea uwezo Wauguzi na Wakuu wa Vituo vya Afya na watoa huduma za afya ngazi ya Jamii.
Hayo yameibainishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mhe.Mwanaidi Ali Khamis katika maadhimisho ya klabu ya Jubilee ya Kina Mama Agosti 16,2025,Jijini Dar es salaam.
Mhe Mwanaidi amefafanua kwamba katika kuimarisha elimu ya malezi chanya kwa Wazazi na Walezi Wizara imendaa Mwongozo unaosisitiza wajibu wa Wazazi katika Malezi ya Watoto na Familia wenye lengo la kuhimiza Wazazi wote wawili kushiriki kikamilifu katika kulea Watoto.
“Kutokana na uwepo wa Mwongozo huo tumeweza kuandaa jumbe maalum za kuelimisha jamii kuhusu upatikanaji wa huduma sahihi za afya, lishe, ulinzi na usalama wa mtoto kulingana na umri na mahitaji yao lakini vile vile elimu ya wajibu wa Wazazi na Walezi katika malezi inaendelea kutolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo Majukwaa ya Dini pamoja na vyombo vya Habari.”Amesema Mwanaidi.
Aidha,Mhe Mwanaidi ameeleza pia juu ya jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo YJamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum inaendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji
wa Program ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi hususani Wanawake ili waweze kufikia malengo kikamilifu na kwa wakati kwa lengo la kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Program hizo ni pamoja na kuratibu utoaji wa mikopo ya Maendeleo ya Wanawake,Mikopo ya Halmashauri, Mikopo ya Wafanyabiashara Wadogo(Machinga) pamoja na kuratibu utoaji mafunzo ya ujasiliamali hivyo tuimarishe ushirikianao uliopo kwa lengo la kuwawezesha Wanawake kupata maarifa na rasilimali zitakazowawezesha kuleaWatoto kwa maslahi ya familia na taifa kwa ujumla kwani tunaamini
Familia Bora ndiyo msingi wa kuwa na Taifa Imara.” Amesema Mwanaidi.