SERIKALI INATEKELEZA MIPANGO MINGI YA USAWA WA KIJINSIA: WAZIRI DKT. GWAJIMA

Na WMJJWM-Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatekekeza mipango mingi ya kuleta usawa wa kijinsia, na kuandaa kizazi kipya cha viongozi wanawake wenye weledi, uthubutu na maono.
Amesema mipango hiyo imeainishwa kwenye Mpango wa Taifa wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) na kuongeza kuwa, Taifa linapojenga viongozi wa kike wa kizazi kipya, linajenga jamii imara, yenye maono na maendeleo endelevu, ambapo juhudi za kuwawezesha wanawake katika uongozi zinahitaji mshikamano wa wadau wote.
Ameyasema hayo leo Februari 11, 2025 jijini Dar Es Salaam wakati akizindua Programu ya Uongozi kwa Wanawake Vijana, iliyoandaliwa na Taasisi za Care International Tanzania pamoja na Mwanawake Initiative Foundation (MIF), inayolenga kuwajengea uwezo wa kushiriki katika vyombo vya kutoa maamuzi viongozi wanawake vijana, wenye umri wa miaka 20 hadi 35.
Dkt. Gwajima amesema Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kukuza uchumi na maendeleo ya Watanzania, hususan kwa vijana na wanawake.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa, bado kuna changamoto kubwa katika ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi huku akitolea mfano
uwakilishi wa wanawake bungeni ni kati ya 36% - 37%, lakini katika ngazi za serikali za mitaa, bado ni mdogo pia.
"Katika sekta binafsi, ni 20% tu ya wanawake wanaoshikilia nafasi za juu za uongozi kama wakurugenzi wakuu (CEOs) au wajumbe wa bodi. Aidha, misingi hasi ya kimila na kitamaduni imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika vyombo vya kutoa maamuzi, siasa, na nafasi za uongozi maendeleo ya uchumi ambapo, hali hii inathibitisha kuwa bado tunahitaji jitihada zaidi na mipango madhubuti ili kuwezesha na kuharakisha uwepo wa usawa wa kijinsia" amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Care International (Tanzania) Bi. Prudence Masako amesema, programu hiyo inalenga kujenga msingi wa wanawake katika taifa hasa katika kuwapa watoto wa kike uwezo wa kuwa Viongozi katika nyanja mbalimbali nchini.
"Uwekezaji katika uongozi wa wanawake vijana sio tu suala la uwakilishi, bali ni suala la utumishi na ujenzi wa Taifa lenye mustakabali bora hivyo, tunapowawezesha wanawake kuongoza, tunahakikisha kuwa, sera zinakuwa jumuishi zaidi, maamuzi yanakuwa na mtazamo mpana na jamii yetu inanufaika zaidi Kwa maana hiyo, leo hatuzindui tu mpango wa uongozi, bali tunazindua harakati za kizazi kipya cha viongozi wanawake watakaobadili historia ya nchi yetu" amesema Bi. Masako.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanamke Initiative (MIF) Mhe. Wanu Hafidh Ameir amesema, mafunzo hayo ni muhimu kwa vijana hasa wa jinsia ya kike kwani yanawaandaa kuwa viongozi muhimu katika ngazi za maamuzi ambapo pia ameishukuru Taasisi ya CARE kwa kushirikiana nao katika kuandaa mafunzo hayo.