SERIKALI INATAZAMA WATOTO WOTE KWA JICHO LA KARIBU.
SERIKALI INATAZAMA WATOTO WOTE KWA JICHO LA KARIBU.
Na Witness Masalu, WMJJWM-Dodoma
Serikali yaendelea kusimamia na kuhakikisha kwamba watoto wote nchini hususani wanaoishi katika mazingira magumu wanafikiwa na kupatiwa huduma stahiki.
Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Nandera Mhando alipofika kusikiliza mashauri ya mtoto aliyeripotiwa katika mtandao wa kijamii kuishi katika mazingira magumu akiwa chini ya uangalizi wa bibi yake leo Desemba 18, 2025 jijini Dodoma.
Dkt. Nandera ameeleza kwamba Serikali ilichukua hatua ya haraka ya kufuatilia hali ya mtoto huyo baada ya kupata taarifa hizo kwa kumtafuta Bibi wa mtoto huyo katika hospitali ya Agha Khan jijini Dodoma.
“Tulifikiri mtoto yupo katika hatari kubwa ya ugonjwa lakini baada ya kufanyiwa uchunguzi ilionekana mtoto ana changamoto ya lishe na Serikali iliona ni vyema kumchukua mtoto huyo na kumpatia lishe bora mpaka atapotimiza miaka miwili.” ameeleza Dkt. Nandera.
Aidha Dkt. Nandera ametoa rai kwa jamii hususani watu wenye nia njema za kusaidia watoto waishio katika mazingira magumu na hatarishi kufuata taratibu za kuwafikia na kuwasaidia walengwa ikiwemo hatua ya awali ya kufika katika mamlaka ya uongozi wa Serikali za mitaa.
“Sheria hairuhusu mtoto yeyote mwenye changamoto au aliye katika mazingira hatarishi kutolewa kwenye vyombo vya habari na endapo mtu ana nia ya dhati ya kusaidia mtoto kusaidiwa inabidi afike kwa uongozi wa Serikali za mtaa na akiona ushirikiano haupo anaweza kwenda ngazi za Wilaya, mkoa mpaka kitaifa lakini si kutumia vyombo vya habari kutangaza shida za watoto” ameeleza Dkt. Nandera.
Awali akizungumza Afisa Ustawi wa jijini Dodoma Rachel Balisidya amesema familia ya Bibi huyo haikua na changamoto za kufikia hatua ya kutangazwa kwenye vyombo vya habari kwani watoto wake wanamhudumia na kushirikiana nae hatua kwa hatua.
“Tumegundua kwamba changamoto iliyopelekea mtoto kukosa lishe ni usimamizi hafifu wa ulaji, kwani baada ya mtoto kufikisha miezi nane hatakiwi kulazimishwa kutumia maziwa ya unga peke yake bali anatakiwa kutumia vyakula vingine, lakini pia mara nyingi Bibi yake amekua akizunguka na mtoto huyo katika maeneo yake ya biashara na kutofuatilia kwa karibu ulaji wa mtoto huyo” amesema Rachel.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Nghongona Leah Mwagama amesema baada ya kusikiliza kwa umakini yaliyozungumzwa na Kamishna wa Ustawi, Bibi wa Mtoto huyo ameridhia kuikabidhi Serikali mtoto huyo ili aweze kupata lishe bora mpaka atapofikiwa miaka miwili.
MWISHO.