Habari
RAIS SAMIA ATOA ZAWADI KWA WAHITAJI SIKUKUU ZA MWISHO WA MWAKA

RAIS SAMIA ATOA ZAWADI KWA WAHITAJI SIKUKUU ZA MWISHO WA MWAKA
*Waziri Gwajima azikabidhi kwenye vituo*
Na WMJJWM, Dar es salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amekabidhi zawadi mbalimbali zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka kwa watu 2056 wenye uhitaji wanaopata huduma kwenye vituo 29 vilivyo kwenye mikoa yote 26 Tanzania Bara. Vituo hivyo vimewakilisha vingine zaidi ya 300 vyenye takribani walengwa 9000.
Akikabidhi mahitaji hayo katika Kituo cha kulea Watoto Yatima cha Hisani, wilayani Kigamboni mkoa wa Dar es Salaam Desemba 20, 2022, Waziri Gwajima ametoa salaam za Mhe. Rais kwa wahitaji wanaotunzwa kwenye vituo vyote nchini wakiwemo watoto na wazee wasiojiweza 263 kwenye makazi 14 ya Serikali na wengine 537 wanaohudumiwa kwenye makazi ya watu binafsi.
Waziri Gwajima amesema utoaji wa mahitaji hayo kwa kituo hicho unazindua rasmi utoaji wa zawadi hizo kwa mikoa yote utakaofanywa na wakuu wa mikoa kwa kushirikiana na wadau wengine watakaoguswa katika maeneo yao au Mikoa yao.
Zawadi hizo ni pamoja na Mchele, Juice, Mafuta ya kupikia, Maharage na vitoweo.
Kwa upande wao, watoto wa kituo hicho kwa niaba ya wahitaji wengine wamemshukuru Samia Suluhu kwa Upendo wake kwao na wanamuombea kwa mwenyezi Mungu maisha marefu ili aendelee kuwatumikia.
MWISHO