Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

PAC YAIPONGEZA TICD UTEKELEZAJI MRADI WA UJENZI JENGO LA UTAWALA

Imewekwa: 25 Mar, 2025
PAC YAIPONGEZA TICD UTEKELEZAJI MRADI WA UJENZI JENGO LA UTAWALA

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeupongeza uongozi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) kwa usimamazi madhubuti wa mradi wa ujenzi wa jengo jipya la utawala.

Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 24, 2025 na Mhe. Japhet Hasunga, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, mara baada ya ziara ya kamati hiyo kutembelea mradi wa ujenzi.

‘’Uongozi wa Chuo pamoja na Wizara {Wizara ya Maeneeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum} mmefanya kazi nzuri ya usimamizi madhubuti wa mradi. Kukamilika kwa mradi kutoboresha utoaji wa huduma kwa watumishi wa Chuo’’, amenukuliwa Mhe. Hasunga.

Kwa upande wake Dkt. Bakari George, Mkuu wa Chuo – TICD ametumia kikao hicho kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia kutolewa kwa fedha zilizowezesha utekelezaji wa mradi.

‘Kukamilika kwa mradi huu kunaenda kutoa majibu ya changamoto ya udogo na uchakavu wa jengo la utawala la sasa, kukosekana kwa ofisi za viongozi, uhaba wa kumbi za mikutano na kuboresha mwonekano na mandhari ya Chuo’’, amenukuliwa Dkt. Bakari akitoa shukrani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Dkt. Bakari George, mradi huo unagharimu kiasi cha shilingi 5,664,000,000, jengo ambalo lina ghorofa tatu (sakafu nne) linalokusudiwa kuwa na ofisi 44 pamoja na kumbi 5 za mikutano zenye uwezo wa kuchukua watu 545 kwa wakati mmoja.

Kupitia ziara hiyo, Mhe. Amir Mkalipa, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, umeupongeza uongozi wa TICD kwa ushirikiano ambao wanautoa kwa wilaya katika kutekeleza shughuli mbalimbali za serikali.