Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA TAIFA SAFI-Dkt Mpango

Imewekwa: 11 Mar, 2025
NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA TAIFA SAFI-Dkt Mpango

Na WMJJWM,Kigoma.

Serikali imeongeza fursa za uwezeshaji wanawake kiuchumi kuanzia ngazi ya Kaya kwa kwa lengo la kuwawezesha kumudu gharama za matumizi ya nishati safi.

Fursa hizo ni pamoja na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kwa makundi ya wanawake asilimia 4, vijana asilimia 4 na watu wenye ulemavu asilimia 2.

Hayo yamebainishwa  leo Machi 03,2025, Mkoani Kigoma na Makamu wa Rais,Dkt Phillip Mpango katika Kongamano kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniania Kanda ya ya Magharibi

“Uunganishaji umeme umefikia Vijiji vyote 12,318 sawa na asilimia 100. Kwa sasa umeme umefikia vitongoji 33,657 kati ya vitongoji 64,359. Aidha, kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji 20,000 imeanza. Maendeleo haya yanachagiza matumizi ya umeme kama moja nishati safi ya kupikia na hivyo kuongeza hamasa kwa jamii katika matumizi ya nishati hiyo na utunzaji wa mazingira.”amesema Dkt Mpango.

 Vilevile,Dkt Mpango ameeleza kuwa ili kukabiliana na changamoto ya matumizi ya nishati isiyo safi, Serikali inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024 – 2034 ambapo mkakati huo unalenga  kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi.

“ katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imetoa Ruzuku kwenye mitungi ya gesi ambapo Wananchi wananunua mitungi ya gesi kwa nusu ya bei ya kuuzia katika maeneo ya Wilayani na Vijiji – Miji. Kwa kipindi cha Septemba 2024 hadi Januari 2025, jumla ya mitungi 78,957 yenye ruzuku iliuzwa kwa Wananchi na bado inaendelea kuuzwa.”amesema Dkt Mpango.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa  Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ametoa rai kwa wanawake kujitokeza kwa wingi katika makongamano yanayofanyika katika kanda zao, Usiku wa Mwanamke na kilele cha maadhimisho.