NIMR YABUNI PROGRAMU YA SIMU INAYOSAIDIA KUBORESHA MALEZI YA WATOTO: WAZIRI GWAJIMA AIPONGEZA

Na WMJJWM - Mwanza
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa kuanzisha mfumo unaotumia Simu (Parenting Application Program) ambao unaosaidia Wazazi na Walezi kupata elimu ya malezi chanya kwa watoto kwa njia ya mtandao (online).
Dkt. Gwajima ametoa pongezi hizo Februari 9, 2025, jijini Mwanza wakati wa kikao kati ya Wizara na NIMR kwa ajili ya kupitia maendeleo ya programu hiyo na kujadili namna ya kupanua wigo wa watumiaji. Pamoja na majadiliano juu ya matokeo na shuhuda za wanufaika wa mfumo huo unaoitwa Parent App.
"Nikiwa Waziri mwenye dhamana ya kusimamia malezi ya watoto na familia, napokea kwa furaha ubunifu huu wa kuongeza thamani katika programu za Wizara. Ni muhimu kuhakikisha elimu ya malezi inawafikia walengwa wengi zaidi kwa njia rahisi na rafiki," amesema Dkt. Gwajima.
Aidha, Waziri Gwajima ameitaka NIMR kuendelea kushirikiana na Wizara kuimarisha tafiti kuhusu malezi chanya na kushiriki kikamilifu katika uratibu wa Wadau wa Kisekta (Multi-Sectoral Parenting Group) (NMPG) ili kuhakikisha programu za malezi zinafuata miongozo na mila na desturi za Kitanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Sebastian Kitiku, ametoa pongezi kwa taasisi ya NIMR kwa kuanzisha Parent App, akisema takwimu zinaonesha programu hiyo imeleta matokeo chanya katika kuboresha malezi. Awaomba wataalam wa NIMR kuendelea kufanya maboresho ili kuhakikisha programu inawafikia wazazi na walezi wengi zaidi.
Naye Dkt. Joyce Wamoyi, Mtafiti Mwandamizi kutoka NIMR, amemshukuru Dkt. Gwajima na kutoa mwongozo wa maboresho kadhaa ya kuwezesha Parent App kupiga hatua zaidi na kutumika rasmi katika malezi ya watoto.
Baadhi ya wananchi walionufaika na programu hiyo wameleza kwa furaha juu ya matokeo chanya waliyopata baada ya kupatiwa mafunzo ya Parent App. Aidha, wameomba Serikali kuwapatia vitambulisho maalum mara baada ya mafunzo ili kuwatambulisha katika jamii na kuwapa nafasi ya kutoa elimu ya malezi kwa uhuru zaidi.