Habari

Imewekwa: Sep, 13 2023

NAIBU WAZIRI MWANAIDI AITAKA JAMII KUVUNJA UKIMYA VITENDO VYA UKATILI

News Images

NAIBU WAZIRI MWANAIDI AITAKA JAMII KUVUNJA UKIMYA VITENDO VYA UKATILI

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis ameitaka jamii kutokukaa kimya na kunyamazia vitendo vya ukatili vinavyotokea ili kuwa na Jamii iliyo salama hasa kwa Wanawake na Watoto.

"Nimefika katika Mkoa huu wa Geita nimepokea taarifa ya Mkoa nimeona masuala ya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto yameshamiri jumla ya mashauri 625 kwa watu wazima na mashauri 133 ya vitendo dhidi ya Watoto yameripotiwa sasa tusikae kimya tupaze sauti tutokomeze ukatili"

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake mkoani Geita Septemba 11, 2023 iliyolenga kufuatilia utekelezaji wa Sera, na Mipango mbalimbali ya Wizara katika Mamlaka ya Mikoa na Serikali za Mitaa nchini.

Aidha amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii kuwasikiliza wananchi katika maeneo yao ili kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali wanazokabilia nazo katika jamii hasa za upatikitanaji wa fursa za kiuchumi na ukatili wa kijinsia.

"Ndugu zangu Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii Rais Samia Suluhu Hassan ameiunda Wizara hii muhimu mtusaidie kuwafikia wananchi kutatua changamoto zao, tuwasaidie wananchi tuwasikilize" alisisitiza Mhe. Mwanaidi

Wakati huo huo Naibu Waziri Mwanaidi amepokea taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika Kata ya Nyamigota na amewasihi wajumbe wa Kamati ya MTAKUWWA kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii ili wawe na uwezo wa kutoka taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na kuilinda jamii

Pia Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Kikundi cha Manyuki Company Grading Rice killichopo Mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro Halmashauri ya Wilaya ya Geita na kuwataka Wanawake kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili waweze kupata fursa mbalimbali za kupata mikopo kwaajili ya kupata mitaji na masoko ya bidhaa wanazozalisha katika vikundi vyao.

Kwa upande Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Geita Karia Rajab Magaro amemuhakikishia Naibu Waziri Mwanaidi kuratibu masuala yote ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii na kuhakikisha Maafisa wa kada hizo wanawafikia wananchi kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika jamii.

"Nakuhakikishia Mhe. Naibu Waziri tutayasimamamia masuala yote ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili wananchi waweze kupata huduma na namna za kupambana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii yetu" alisema Magaro.

Pia Naibu Waziri Mwanaidi ameihamasisha Jamii kutumia fursa ya Kituo cha Huduma kwa Mteja Jamii Call Center kilicho katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kupiga namba 026-2160250 au 0734 986 503 kwa elimu, msaada na changamoto mbalimbali za wananchi.

Nao baadhi ya Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita wameishukuru Wizara kwa kufuatilia utekelezaji wa Afua mbalimbali na kuiomba Serikali kuendelea kuongeza nguvu katika kuihudumia Jamii hasa kuongeza wingi wa Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii katika Kata na Vijiji.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis yupo katika ziara mkoani Geita kufuatilia utekelezaji wa Sera, na Mipango mbalimbali ya Wizara.

MWISHO