Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MWONGOZO WA URATIBU WA WAJANE NCHINI WAJA.

Imewekwa: 26 Feb, 2025
MWONGOZO WA URATIBU WA WAJANE NCHINI WAJA.

Na WMJJWM - Dar Es Salaam 

Serikali inaendelea kuweka utaratibu mzuri kuhakikisha wajane wanapata haki zao ambapo imeandaa  rasimu ya  mwongozo wa utaribu wa wajane ambao utasaidia Wanawake kupata haki zao ikiwemo haki ya urithi na umiliki wa ardhi baada ya kufiwa na wenzi wao. 

Hayo yamesemwa leo tarehe 21 Februari, 2025 Jijini Dar esa Salaam na Mkurugenzi Msaidizi  wa Idara ya Jinsia  Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Juliana Kibonde  wakati anafungua kikao kazi cha kupitia na kuthibitisha mwongozo wa uratibu wa wajane nchini. 

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina jumla ya wajane zaidi ya milioni 1.3, hivyo Serikali imeandaa mwongozo huo ili kuweka mfumo imara wa uratibu wa wajane katika Jamii  kuanzia ngazi ya Mtaa utakaosaidia  kuachana na Mila na desturi kandamizi kama vile kunyang'anya wajane mali, kuozesha watoto wa kike katika umri mdogo, Vitendo ambavyo vinawaathiri Wanawake kujikwamua kifikra, kiuchumi na maendeleo ya kijamii.

"Wito wangu ni kuhakikisha tunapitia rasimu  ya mwongozo huu na kutoa maoni ya kuboresha kwa lengo la kusaidia Wajane  kuondokana na changamoto zinazowakabili ili kukuza Ustawi wa Mendeleo ya familia zao na taifa kwa Ujumla" Amesema Juliana.

Kwa upande Mkurugenzi wa Taasisi ya RACAS Jacqueline Mhegi ameipongeza serikali  kwa jitihada zake za kutafutia mwarubaini wa kuwapambania Wajane kupata haki zao.

Kukamilika kwa mwongozo wa uratibu wa wajane kutawezesha vyombo mbalimbali vya serikali na viongozi wa kimila kutatua  migororo ya kifamilia kwa misingi ya haki na usawa.