Habari

Imewekwa: Dec, 14 2020

MSIFIKIRIE ZAIDI KAZI OFISINI - DKT. JINGU

News Images

Wahitimu wa taaluma ya Maendeleo ya jamii Monduli wametakiwa kugeuza changamoto zilizopo kwenye jamii kuwa fursa za kupata ajira badala ya kufikiria kufanya kazi ofisini.

Akizungumza katika mahafali ya 11 ya chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema kazi ya Maendeleo ya jamii ni kazi ya vitendo zaidi kuliko ofisini.

Jingu amesema kuwa programu zilizoanzishwa na vyuo vya Maendeleo ya Jamii zinawezesha wahitimu kuwa na uwezo wa kujiajiri na kufanya vizuri katika jamii.

"Kuna baadhi ya maeneo tumeona mabadiliko makubwa kutokana na wahitimu wa chuo hiki waliyofanya kwenye jamii na wao kupata ajira, hivyo tusifikirie wote kufanya kazi ofisini, kwa uzoefu wangu kazi ya Maendeleo ya jamii ni ya "field" zaidi kuliko kukaa ofisini" amesema Jingu.

Amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kuwekeza katika chuo hicho pamoja na vyuo vingine kuhakikisha vinatoa mchango mkubwa katika nchi yetu.

Naye Mkuu wa Chuo hicho Elibariki Ulomi ameeleza kuwa wameendelea kuwa chachu ya mabadiliko kwenye jamii inayowazunguka kwa kufuata miongozo na maelekezo ya Wizara.

Ameongeza pia kuwa wameweza kuhamasisha ujenzi wa makazi bora na uandikishaji wa wanajamii zaidi ya 200 kwenye bima ya Afya.

Wahitimu katika risala yao wameshukuru kwa mafunzo waliyopata kwani yatawasaidia kujiajiri kwani wameandaliwa vizuri.

Jumla ya wanafunzi 430 wamehitimu katika ngazi mbalimbali za taaluma ya maendeleo ya Jamii kwenye chuo hicho.