Habari

Imewekwa: Nov, 26 2020

MILA NA DESTURI CHANYA NI CHANZO KUKABILIANA NA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO-UTAFITI

News Images

Imeelezwa kuwa, mila na Desturi chanya ikiwemo ya kuwapa fursa watoto wa kike kupata elimu kabla ya kuolewa zinatakiwa kuendelezwa katika jamii ili kujenga maadili mema na kutokomeza ukatili kwa Wanawake na Watoto.

Hayo yamebainika katika taarifa ya utafiti uliofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la UNFPA kwa lengo la kuangalia mila na desturi zinavyochangia katika masuala ya ukatili kwa wanawake na watoto nchini, katika kikao cha wadau wanaotekeleza Mpando wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika nyanja ya Mila na Desturi, kilichofanyika leo jijini Dodoma.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo mmoja wa wataalam Dkt. Mathew Senga alisema kuwa, utafiti umebaini kuwa, pamoja na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kuonekana kuongezeka lakini kuna mabadiliko ya uelewa katika jamii kutambua kuwa kuna baadhi ya mila zinazochangia kuongezeka kwa ukatili.

Dkt. Senga amesema uelewa huo kwa jamii unatokana na utekelezaji wa afua mbalimbali zinazolenga kutokomeza vitendo vya Ukatili katika jamii.

Aidha, amesema utafiti umeonesha kuwa hatua zinazochukuliwa katika jamii zimesaidia kubadili mitazamo katika mila na desturi ambazo zinasaidia kupunguza ukatili kwa wanawake na watoto ikiwemo kuongezeka kwa upatikanaji wa elimu, ushirikishwaji wa watoto wa kiume na wanaume katika majadiliano, upashanaji habari kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, upatikanaji wa huduma za Sheria na uwezeshaji wanawake kiuchumi.

Ameongeza kuwa utafiti huo umefanyika katika mikoa saba ya Tanzanja Bara na Visiwani na maoni ya wadau yatachangia kuwezesha matokeo yake kutumika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Vickness Mayao amesema Serikali inaendelea kusimamia Sheria mbalimbali na kuandaa miongozo yenye lengo la kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto ikiwemo utekelezaji wa MTAKUWWA wa mwaka 2017/18 - 2021/22 ambao moja ya maeneo ya kushughulikia ni pamoja kuwezesha jamii kuondokana na mila na desturi zisizofaa katika jamii.

“Kama tunavyofahamu nchi yetu ina zaidi ya makabila 120 yenye mila na desturi tofauti kutoka kabila moja hadi lingine, hata hivyo kuna mila chanya na hasi katika kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto"

"Hivyo mpango wa MTAKUWWA unalenga kuendeleza mila chanya katika jamii zenye lengo la kujenga maadili na kuchochea mabadiliko ya fikra katika jamii” alisema.

Baadhi ya wadau wanaotekeleza Mpango huo katika eneo la Mila na Desturi Anna Fisoo na Francis Selasini wakichangia maoni yao, wameshukuru Serikali na UNFPA kwani kutokana na matokeo ya utafiti huo na kuahidi watayafanyia kazi katika maeneo yao, pia wamesema utafiti huo umewafungua macho kuona maeneo mengine ambayo waliona ni vikwazo katika kutekeleza majukumu yao.