Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

DKT. JINGU AITAKA JAMII KUWATUNZA WAZEE IKIWEPO KUPINGA VITENDO VYA UKATILI DHIDI YAO, AWASHAURI VIJANA KUJIANDAA NA UZEE

Imewekwa: 04 Jul, 2025
DKT. JINGU AITAKA JAMII KUWATUNZA WAZEE IKIWEPO KUPINGA VITENDO VYA UKATILI DHIDI YAO, AWASHAURI VIJANA KUJIANDAA NA UZEE

‎Na WMJJWM – Mwanza

‎Julai 03, 2025 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, ametembelea Kituo cha Wazee cha Bukumbi kilichopo jijini Mwanza, kwa lengo la kuwajulia hali wazee wanaoishi katika kituo hicho pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili.

‎Katika ziara hiyo, Dkt. Jingu amesisitiza umuhimu wa jamii kushiriki kikamilifu katika kuwatunza wazee wao, akibainisha kuwa wazee wana nafasi kubwa katika jamii na wanapaswa kupewa heshima, uangalizi na haki zao kulindwa. Amehimiza pia wazee kushiriki katika Uchaguzi Mkuu pamoja na fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo zile zinazotolewa kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA). Vilevile, amesisitiza kupinga vikali vitendo vyote vya ukatili dhidi ya wazee, akieleza kuwa ulinzi wao ni jukumu la kila mmoja.

‎Dkt. Jingu ametoa wito mahsusi kwa vijana na jamii kwa ujumla kujiandaa kwa maisha ya uzee kwa kutumia vizuri rasilimali walizonazo wakiwa bado vijana. Amesema ni muhimu vijana wawe na mtazamo wa muda mrefu kwa kuwekeza katika familia, mahusiano mema na miradi ya kiuchumi ambayo itawasaidia wanapoingia uzeeni. "Ujana ni hatua ya maandalizi ya uzee, tusikimbie wajibu huu," amesisitiza.

‎Katika hatua nyingine, Dkt. Jingu ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mahabusu ya watoto jijini Mwanza, ambapo ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa, kwani mradi huo umefikia asilimia 90 ya utekelezaji. Ujenzi wa mahabusu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume Maalum iliyoundwa ili kuboresha taasisi za haki jinai nchini, hususan zinazohusiana na watoto.