MDEMU AWATAKA WANUFAIKA WA MKOPO WA WDF KUREJESHA KWA WAKATI
Na Saidi Said, WMJJWM – Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, amewataka wanufaika wa mikopo ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kutoa fursa kwa wanawake wengine wengi zaidi kunufaika na mfuko huo.
Mdemu ametoa wito huo Desemba 15, 2025 wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Dodoma iliyolenga kukagua maendeleo ya vikundi vya wanawake wajasiriamali.
Akizungumza na wanufaika wa mikopo hiyo, Mdemu amewapongeza wanawake hao kwa maendeleo mazuri ya miradi yao, huku akiwakumbusha umuhimu wa kuendelea kurejesha mikopo kwa wakati.
Amesema urejeshaji mzuri wa mikopo ni msingi muhimu wa uendelevu wa mfuko wa WDF, kwani fedha hizo ni za mzunguko na zinalenga kuwainua wanawake wengi kiuchumi.
Katika ziara hiyo, Mdemu amepata fursa ya kutembelea kikundi cha Five Dadas kinachojishughulisha na utengenezaji wa mikate, Kemmy Group kinachojihusisha na usindikaji wa vyakula na viungo kwa matumizi ya nyumbani, pamoja na mjasiriamali Neema Woisoo anayejihusisha na utengenezaji wa juisi na uendeshaji wa mgahawa wa chakula. Katika maeneo hayo, aliwapongeza kwa ubunifu na bidii waliyoionyesha katika kuendesha shughuli zao.
Aidha, Mdemu amewasisitiza wajasiriamali hao kuongeza ubora wa bidhaa zao na kuzingatia upatikanaji wa masoko ili kukuza kipato chao na kuimarisha biashara zao.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa mafunzo na usimamizi kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali ili kuhakikisha mikopo ya WDF inaleta matokeo chanya yanayotarajiwa.
Kwa upande wao, wajasiriamali walionufaika na mikopo hiyo wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mikopo hiyo wakisema imewasaidia kuanzisha na kupanua biashara zao, kuongeza kipato cha familia, kutoa ajira kwa wengine na kuboresha maisha yao kwa ujumla, hivyo kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa.
"Tunaahidi kuendelea kusimama vyema biashara zao pamoja na kurejesha mikopo hiyo kwa wakati, ili kuwawezesha wanawake wengine wengi zaidi kunufaika na mfuko huo". amesema mmoja wa Mjasiriamali
MWISHO