Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MALEZI BORA YA WATOTO NI MSINGI WA TAIFA IMARA - WAZIRI DKT. GWAJIM

Imewekwa: 07 Mar, 2026
MALEZI BORA YA WATOTO NI MSINGI WA TAIFA IMARA - WAZIRI DKT. GWAJIM

Na WMJJWM – Dar es Salaam

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha taasisi ya familia ili kujenga jamii yenye maadili na Taifa imara. Dkt. Gwajima amesema hayo katika Kongamano la Wanawake la “Sisi ni Tanzania: Familia Yangu, Nchi Yangu,” lililofanyika Machi 6, 2026 katika Ukumbi wa Maktaba Mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akizungumza katika kongamano hilo, Dkt. Gwajima ameeleza kuwa malezi bora ya watoto, hasa katika umri wa chini ya miaka mitano, ni muhimu kwa maendeleo ya akili na tabia zao, kwani katika kipindi hicho ubongo wa mtoto hukua kwa kiwango kikubwa. Aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata huduma bora za afya, lishe sahihi, ulinzi dhidi ya ukatili pamoja na mazingira mazuri ya kujifunza na kucheza ili kukuza uwezo wao.

Aidha, ameonya kuwa migogoro ya kifamilia, mmomonyoko wa maadili pamoja na matumizi mabaya ya teknolojia na mitandao ya kijamii vimekuwa vikichangia changamoto kwa watoto na vijana, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na kujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo.

Katika kuimarisha familia na malezi bora, Waziri Gwajima amesema Serikali inaendelea kushirikiana na viongozi wa dini, wadau pamoja na vyombo vya habari kutoa elimu ya malezi chanya, sambamba na kuendeleza kampeni ya “Sisi ni Tanzania” inayolenga kukuza uzalendo, maadili na mshikamano katika jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dkt. Joyce Nyoni, amesema familia ndiyo msingi wa ukuaji na malezi ya watoto, kwani namna wazazi wanavyowalea watoto wao ndiyo huamua tabia na mwenendo wao katika jamii.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Gwakisa Mlawa, amesema lengo la kongamano hilo ni kuwajengea wanawake uwezo, kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi na maamuzi, pamoja na kuendelea kuhimiza usawa wa kijinsia katika jamii, ameongeza kuwa TBC, kama shirika la utangazaji la umma, itaendelea kutumia majukwaa yake ya utangazaji kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu usawa wa kijinsia, pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali