Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MAAFISA MAENDELEO YA JAMII TUTUMIE PIKIPIKI KUONGEZA UFANISI KAZINI-MDEMU

Imewekwa: 24 Oct, 2025
MAAFISA MAENDELEO YA JAMII TUTUMIE PIKIPIKI KUONGEZA UFANISI KAZINI-MDEMU

MAAFISA MAENDELEO YA JAMII TUTUMIE PIKIPIKI KUONGEZA UFANISI KAZINI-MDEMU

 

Na Mwandishi Wetu WMJJWM-Rukwa

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Rukwa kuzitumia pikipiki waliokabidhiwa ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

Mdemu ameyasema hayo tarehe 24 Oktoba, 2025 wakati akikabidhi pikipiki 8 kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri za Mkoa wa Rukwa.

 

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inakabidhi pikipiki nane (8) kwa Halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa kwa ajili ya Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata hatua inayolenga kuwawezesha maafisa hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi.

 

Mdemu amebainisha kuwa pikipiki hizo ni nyenzo muhimu za kazi zitakazorahisisha mawasiliano na ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo katika maeneo ya vijijini na Kata. Amesema kuwa Serikali imekusudia kuongeza ufanisi wa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya maendeleo, kuimarisha ushiriki wa jamii katika miradi ya kijamii, na kuchochea uwajibikaji katika ngazi za chini za utawala.

 

Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Daudi Sebyiga, amepongeza hatua hiyo akieleza kuwa itaboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa sekta ya maendeleo ya jamii katika Halmashauri za Mkoa wa Rukwa huku akisisitiza kuwa pikipiki hizo zitaongeza kasi ya utoaji huduma na kufikisha elimu ya maendeleo kwa wananchi kwa wakati.

 

Nao Maafisa Maendeleo ya Jamii waliopokea pikipiki hizo wameishukuru Serikali ya kwa kuwapatia vyombo hivyo vya usafiri, wakibainisha kuwa vitasaidia kupunguza changamoto ya usafiri na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao katika maeneo ya vijijini.

 

MWISHO