MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KUWENI CHACHU YA MABADILIKO KWA JAMII- DKT. GWAJIMA

Na WMJJWM - IRINGA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwaelimisha wananchi juu ya fursa mbalimbali zinazoweza kuboresha maisha yao.
Akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Maafisa Maendeleo ya Jamii mkoani Iringa, Februari 22, 2025, Dkt. Gwajima amesema kazi ya Serikali sio kutunga sera pekee bali kuibua fursa na kuwawezesha wananchi.
"Dhamira ya serikali ni kuhakikisha jamii zinapiga hatua kimaendeleo. Kazi yenu haipaswi kuwa kutekeleza sera pekee, bali kubuni na kusaka fursa zitakazosaidia wananchi kushinda changamoto zao za kiuchumi na kijamii," alisema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima pia amekumbusha umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya Siku ya Wanawake Duniani itakayoadhimishwa tarehe 8 Machi, 2025. Aliwataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanawahamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa siku hiyo.
"Ninawaomba mshiriki kikamilifu katika shughuli zote za maadhimisho zitakazofanyika katika maeneo yenu, ikiwemo makongamano ya Kanda mbalimbali. Pia, shirikianeni na majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ili waweze kushiriki ipasavyo na kufanikisha malengo yetu ya kuwawezesha wanawake," alisema Waziri Gwajima.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Bi. Doris N. Kalasa, amesema kuwa kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuwajengea uwezo Maafisa Maendeleo ya Jamii ili kuongeza ufanisi wao katika kutekeleza majukumu yao.
"Nina imani kwamba kongamano hili limewapatia maarifa mapya na mbinu bora za kusimamia maendeleo ya jamii kwa weledi na uaminifu. Nendeni mkayatumie kwa vitendo ili kuleta mabadiliko chanya," alisema Bi. Kalasa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, amemshukuru Waziri Dkt. Dorothy Gwajima kwa jitihada zake katika kukuza ustawi wa jamii na kupambana na ukatili wa kijinsia, akisisitiza kuwa amekuwa chachu ya mabadiliko kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii.
"Mheshimiwa Waziri, tunatambua na kuthamini mchango wako mkubwa katika kuhakikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii wanapata mwongozo sahihi wa kuboresha maisha ya wananchi.