KIZAZI CHENYE USAWA NI CHACHU YA MAENDELEO -RAIS. DKT. SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaendelea kuweka Sera na Sheria zinazoleta matokeo chanya katika Jamii hasa kwa maeneo ya kutetea haki za Wanawake ili kuleta usawa wa kijinsia.
Rais Samia ameyasema hayo leo tarehe 8, Machi 2025, jijini Arusha wakati akihutubia katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Mhe. Dkt. Samia amesema Tanzania imepiga hatua katika utekelezaji wa azimio la Beijing ambalo limependekeza kuwepo kwa haki sawa na kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya Wanawake.
"Natamani kuona mabadiliko ya Sheria na sera tunazoziridhia zinaleta matokeo chanya kwa watu wote, kama vile haki ya ya kumiliki ardhi kwa Wanawake" amesema Dkt. Samia.
Aidha, Dkt. Samia ameeleza kwamba Maendeleo ya nchi yanajengwa kwa mshikamano kati ya Wanawake na wanaume kwa kuheshimu Sheria na miongozo ya uwezeshaji Wanawake kiuchumi.
Amehimiza Wanawake kuendelea kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali katika mihimili ya maamuzi Serikalini na sekta binafsi ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili Wanawake nchini.
"Tanzania tumepiga hatua kubwa katika kuleta usawa wa kijinsia kwenye taasisi za Kiserikali, sekta binafsi na Siasa tuna Viongozi wa ngazi za juu katika mihimili ya kufanya maamuzi" amesema Dkt. Samia.
Pamoja na hayo ameitaka jamii kuhakikisha inajenga kizazi cha watoto wanaojiamini na wenye uwezo wa kujenga hoja, vijana ambao watatambua ukubwa wa hoja zao si ukali wa sauti wala maneno.
Awali, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema wiki ya makongamano ya kikanda imekuwa na mafanikio ambapo kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi na huduma mbalimbali za kijamii zimetolewa, huku wananchi wengi wakipata msaada wa Kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Dkt Gwajima ametoa wito kwa Wanawake kuendelea kumuunga mkono Rais Samia katika jitihada anazozifanya kuimarisha Ustawi na Maendeleo ya Wanawake kiuchumi.