Habari

Imewekwa: Mar, 20 2023

​KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA TENGERU MATUMIZI MAZURI YA FEDHA

News Images

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo na Ustawi wa Jamii, imeipongeza Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa matumizi mazuri ya fedha kwenye mradi wa Bweni la wanachuo lililogharimu sh. Bil. 2.7.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa Mradi huo, Mwenyeki wa Kamati hiyo Mhe. Fatuma Toufiq amesema Kamati imeridhishwa na Ujenzi wa Bweni hilo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 500 kwa wakati mmoja.

"Kama Wajumbe wa Kamati, lazima tuseme ukweli tumeridhishwa sana na kazi hii, tunampongeza sana Mkuu wa taasisi na Watendaji wake wote kwa Moyo wa Kizalendo walioubeba kuhakikisha Thamani ya fedha ya Serikali inaonekana kwenye Mradi huu" amesema Mhe. Toufiq.

Naye mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo Mhe. Katani Ahmed Katani amesema Mkuu wa Chuo hicho ni mfano wa kuigwa katika ujenzi wa miradi hiyo.

Awali akisoma taarifa ya mradi, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu, ameishukuru Serikali kwa kutoa shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo na shilingi bilioni 1.6 ya ununuzi wa samani na vifaa vya TEHAMA.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo, Janeth Zemba amewahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa chuo kitaendelea kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya chuo ikiwemo mabweni ya wanafunzi na nyumba za watumishi.

Taasisi hiyo ina jumla ya wanafunzi 2918, kwa mwaka wa masomo 2022/2023 ambapo 1952 (66.8%) ni wanawake na 966 (33.2%) ni wanaume.

MWISHO