Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR YAVUTIWA NA MIRADI YA MAKAO YA WATOTO KURASINI

Imewekwa: 15 Apr, 2025
KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR YAVUTIWA NA MIRADI YA MAKAO YA WATOTO KURASINI

Na WMJJWM- Dar Es Salaam

Kamati ya Ustawi wa Jamii, Baraza la Wawakilishi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Sabia FilFil Sane imetembelea miradi mbalimbali iliyopo katika Makao ya Taifa ya Watoto Kurasani ikiwa ni ziara ya kujifunza jinsi ambavyo vituo vya kulelea watoto vya Tanzania Bara vinavyoshughulika na suala la malezi ya watoto.

Akizungumza katika ziara hiyo iliyofanyika Aprili 14, 2025 Mwenyekiti wa Kamati hiyo Sane amefurahishwa na uendeshaji wa Makao hayo kwa namna ambayo watoto wanalelewa na kujifunza stadi mbalimbali za kazi mbali ma elimu ya darasani wanayopata wakiwa katika hatua mbalimbali shuleni.

Ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa juhudi zake za kuendesha Makao hayo ambayo yanasadia watoto ambao wanaoishi katika mazingira hatarishi na magumu kupata huduma muhimu ikiwemo elimu afya na Malezi kama watoto wengine waliopo katika familia.

Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Mhe. Anna Athanas Paul amesema Wizara hiyo imejifunza mbinu mbalimbali za uendeshaji wa Makao ya Watoto kutoka katika Makao hayo na itaenda kuzitumia katika kuboresha uendeshaji wa Makao kwa upande wa Zanzibar ikiwemo kuanzisha miradi mbalimbali katika Makao ya Watoto yanaendeshwa na Serikali.

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando amesema Wizara imefarijika kupata ugeni kutoka kwa Kamati ya Baraza la Wawakilishi na Uongozi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar kutembelea Makao ya Watoto Kurasini na kujifunza masuala mbalimbali yanayofanyika
katika Makao hayo.

Aidha kamati iliipongeza Makao hayo kwa na hatua iliyochukua ya kuanzisha miradi ya kimaendeleo ambayo ni mradi wa ufugaji wa kuku na mradi wa kilimo cha mbogamboga.