HUDUMA KWA MANUSRA WA UKATILI ZAIMARISHWA NCHINI.

Na WMJJWMM, Dodoma.
Serikali imeendelea kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupitia afua mbalimbali ikiwemo Mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) kwa kutoa huduama za afya kisaikolojia, kijami na kisheria kwa manusura
Hayo yamesemwa leo Februari 17,2025,Mkoani Dodoma na Kamishna msaidizi wa Ustawi wa Jamii, Tulo Masanja katika Kikao cha Utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) eneo la Huduma kwa Manusura wa Vitendo vya Ukatili.
Masanja amesema kuendelea kujitokeza kwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ni kiashiria hai kwamba bado kuna uhitaji wa kuimarisha huduma kwa manusura ikiwemo huduma za kiafya,Kisaikolojia na kisheria .
“Licha ya serikali kufanikiwa kuimarisha huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi, huduma za makazi ya Muda kwa manusra wa vitendo vya ukatili, kuwaaunganisha watoto na familia, Utoaji wa mafunzo ya huduma ya afya ya akili na msaada wa kisaikolojia na uimarishaji wa mifumo ya utoaji wa huduma, bado kuna uelewa mdogo kwa manusura kuhusu haki za kijamii, kiuchumi na kisheria" amesema Masanja.
Kutokana na hali hiyo Serikali inaendelea kuelimisha jamii juu ya haki za wanawake na watoto, kwa kushirikiana na viongozi wa dini na mila ili kuhakikisha jamii inaachana na mila na desturi zenye madhara na kukuza utamaduni wa kulinda haki za binadamu.
Aidha mratibu wa dawati la huduma za manusra wa ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto kutoka wizara ya Afya, Desteria Manyanga amesema huduma zinazopatikana katika nyumba salama ni pamoja na kuwapatia dawa za kuzuia maambukizi ya ukimwi au mimba endapo amebakwa na kuhakikisha manusura anapata matibabu msaada wa kisaikolojia.
Kwa upande wake mwakilishi wa shirika linaloshughulika na masuala ya watoto (UNICEF) Tanzania, Evance Emori amesema shirika hilo linaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha kila mtoto analindwa na kupata haki zake za msingi.