ELIMU YA MAENDELEO YA JAMII NI CHACHU YA AJIRA NA KUJITEGEMEA: NAIBU WAZIRI MARYPRISCA
Na Jackline Minja WMJJWM
Iringa
Vyuo vya maendeleo ya jamii vimetajwa kuwa ni mhimili muhimu wa mabadiliko ya fikra, uundaji wa ajira na ustawi wa wananchi, hasa katika ngazi ya msingi ambako changamoto za kiuchumi na kijamii zinapoanzia ambapo mwelekeo huo umetajwa kuwa suluhisho la kupunguza utegemezi, kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo yao wenyewe.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati akizungumza na wanachuo pamoja na watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kilichopo mkoani Iringa tarehe 13 Desemba 2025.
Mhe. Maryprisca amesema mafanikio ya Chuo hicho katika kudahili wanafunzi 2,571 ndani ya kipindi cha miaka minne yanaonesha mchango wake mkubwa katika kuandaa rasilimali watu yenye tija kwa Taifa.
“Vyuo vinapaswa kuandaa wahitimu wenye uwezo wa kujitegemea, kuajiri wengine na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii zao, huu ni ushahidi kuwa elimu inayotolewa hapa inaendana na mahitaji ya nchi na inawaandaa wahitimu kuwa waajirika, wajiajiri na wawezeshaji wa maendeleo ya jamii,” amesema Mhe. Maryprisca
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha Godfrey Mafungu amesema Chuo kinaendelea kutekeleza mafunzo yanayolenga kumwandaa mwanafunzi kuwa watatuzi wa changamoto za jamii kwa kuunganisha nadharia na vitendo ambapo kupitia programu za kitaaluma, tafiti na miradi ya uzalishaji mali, Chuo kimefanikiwa kuwajengea wanafunzi ujuzi unaowawezesha kuajirika, kujiajiri na kuchangia maendeleo ya jamii wanazotoka.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi, rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho Abasi Kibwana Jumanne, ameishukuru Wizara na uongozi wa Chuo kwa kuweka mazingira yanayowawezesha wanafunzi kupata elimu inayozingatia ujuzi wa vitendo na mahitaji ya jamii
“Ziara hii imeongeza ari na motisha kwa wanafunzi katika kujifunza na kuwahudumia wananchi kwa weledi pindi watakapohitimu maana tumejipanga kusoma kwa bidii, kuzingatia maadili na kutumia elimu tunayopata hapa kuwa chachu ya maendeleo katika jamii zetu” amesema rais wa Chuo.
MWISHO