ELIMU MLIYOIPATA IKAWE SULUHISHO LA CHANGAMOTO KATIKA JAMII – MHE. MAHUNDI
ELIMU MLIYOIPATA IKAWE SULUHISHO LA CHANGAMOTO KATIKA JAMII – MHE. MAHUNDI
Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mbeya (CUoM) kutumia elimu waliyoipata kuisaidia jamii kuleta mabadiliko na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Mhe. Mahundi ameyasema hayo wakati wa mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mbeya (CUoM), ambapo jumla ya wahitimu 2,819 wamehitimu katika kada mbalimbali.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mhe. Mahundi amesema
Serikali itaendelea kuongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu ili kupanua fursa kwa vijana wengi zaidi kupata elimu, huku akiwapongeza wazazi, walezi na wafadhili kwa mchango wao uliowawezesha wahitimu kukamilisha masomo yao.
“Elimu mliyoipata si kwa ajili yenu pekee, bali ni dhamana ya kuisaidia jamii na kuchangia maendeleo ya Taifa. Serikali itaendelea kuongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu ili vijana wengi zaidi wapate fursa ya kusoma na kujiandaa kujitegemea badala ya kusubiri ajira.”amesema Naibu Waziri Mahundi
Naye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha CUoM, Profesa Romward Haule, amesema Chuo hicho kimeendelea kupokea maombi mengi ya kujiunga kutokana na ubora wa wakufunzi, miundombinu ya kisasa pamoja na vifaa bora vya kufundishia na kujifunzia huku akibainisha kuwa Chuo kinaendelea kuboresha mitaala yake ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi, maadili na uwezo wa kujiajiri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha CUoM, Godfrey Mwasekaga, amewataka wahitimu kujikita katika ujasiriamali na ubunifu, badala ya kusubiri ajira rasmi, huku akiomba Serikali kuendelea kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini kupata fursa zaidi za elimu ya juu.
MWISHO