DKT. GWAJIMA AHIMIZA VIONGOZI KUTATUA CHANGAMOTO MIKOPO KWA WANAWAKE
DKT. GWAJIMA AHIMIZA VIONGOZI KUTATUA CHANGAMOTO MIKOPO KWA WANAWAKE
Na WMJJWM – Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii kote nchini kuhakikisha wanafuatilia kwa kina changamoto zinazowakabili wanawake katika upatikanaji wa mikopo inayotolewa na Serikali ikiwemo mikopo inayotolewa kwa Sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na kuchukua hatua zaidi za kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo Desemba 18, 2025, akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi Wilaya ya Ubungo mkoani Dar Es Salaam, alipotembelea Kikundi cha Wanawake cha Mama Kwanza ambacho kinakabiliwa na changamoto ya mtaji wa shilingi milioni sita ili mradi wao uanze kufanya kazi kikamilifu changamoto iliyotokana na sababu za kiufundi wakati wa uchambuzi wa andiko la mradi huo.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Gwajima ametoa maagizo kwa watendaji wa Wilaya hiyo kuhakikisha ndani ya siku kumi changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi na kikundi hicho kinapatiwa fedha hizo ili kuwawezesha kuanza uzalishaji wa mafuta ya mawese.
Aidha, Dkt. Gwajima amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kote nchini kuwa karibu na jamii na kutoa ushirikiano wa dhati kwa wananchi huku akisisitiza kuwa changamoto nyingi zinazowakabili wanawake ziko ndani ya uwezo wa wataalamu hao na hazihitaji kila mara kuhusisha uongozi wa juu endapo kutakuwepo mawasiliano ya karibu, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Ninaagiza ndani ya siku kumi, wiki ya kwanza ya mwezi Januari, nipokee taarifa kwamba Mkurugenzi wa Halmashauri kwa mamlaka aliyonayo, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, mmepata ufumbuzi wa tatizo hili na hawa wanawake wamepatiwa shilingi milioni sita” amesema Dkt. Gwajima.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando, amesema amepokea maelekezo ya Waziri na kuahidi kuyatekeleza kwa kushirikiana na wataalamu wa halmashauri pamoja na viongozi wa kata na mitaa, ili kuhakikisha changamoto za Kikundi cha Mama Kwanza pamoja na vikundi vingine vinavyokabiliwa na changamoto kama hizo zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Kwa upande wa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, wameahidi kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wakiwemo Mkurugenzi wa Manispaa na watendaji wa kata, ili kuhakikisha kikundi hicho kinapatiwa fedha zinazostahili, sambamba na kutoa usaidizi wa kitaalamu ili mradi huo uanze kufanya kazi na kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wanakikundi.
MWISHO