Habari

Imewekwa: Sep, 15 2023

BUHARE YAHIMIZWA KUKAMILISHA UJENZI WA MIUNDOMBINU

News Images

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe Mwanaidi Ali Khamis amekitaka Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare kukamilisha mradi wa ujenzi wa jengo la mihadhara ili kuwezesha wanafunzi wengi wa fani ya Maendeleo ya Jamii kupata nafasi ya masomo.

Ameyasema hayo Wilayani Musoma Mkoani Mara Septemba 14, 2023 alipotembelea na kukagua ujenzi huo unaogharimu shillingi Millioni 50 mpaka kukamilika kwake.

Naibu Waziri Mwanaidi amesema, kukamilika kwa jengo hilo ni chachu ya kuongezeka kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao upatikanaji wake bado ni changamoto hasa kwa ngazi ya Kata na Mitaa.

Mwanaidi amesema, Serikali imetoa fedha ili kuboresha Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Wizara na kuvifanya kuwa na mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.

"Sisi kama Wizara tunaendelea kuboresha miundombinu katika Vyuo tunavyovisimamia ili tuwe na Vyuo vitakavyozalisha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wenye weledi na ufanisi" alisisitiza Naibu Waziri Mwanaidi.

Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare Paschal Mahinyila amesema Chuo hicho kimefanikiwa kufanya mambo mbalimbali katika jamii ikiwemo tafiti ya namna ya kupambana na vitendo vya ukatili, kuhamasisha Jamii kwenye masuala yahusuyo utunzaji mazingira, ujenzi wa Makazi bora na kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

Awali akisoma taarifa ya Mradi huo Makamu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare Benard Ndiege amesema jengo hilo linajengwa kwa kutumia utaratibu wa kuwatumia wakandarasi wa ndani (force account) na litatatua changamoto za upungufu wa Majengo kwa ajili ya kumbi za mihadhara Chuoni hapo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea wazee wanaoishi katika Makazi ya Wazee Nyabange yaliyopo Manispaa ya Musoma na kuwaahidi kutatua changamoto ikiwemo uchakavu wa miundombinu iliyopo.

Vilevile Naibu Waziri Mwanaidi ametembelea Makao ya Watoto Jipe Moyo yanayotunza Watoto walio katika mazingira hatarishi na waliokimbia vitendo vya ukatili hasa ukeketaji huku akiwaasa wadau kuendelea kushirikiana na Serikali kuwasaidia watoto hasa wa kike walio katika mazingira magumu ili wapate sehemu salama ya kukaa na kujiendeleza.