BILIONI 262 ZA MRADI WA PAMOJA KUKUZA USAWA WA KIJINSIA NA USATWI WA JAMII NCHINI.
Na WMJJWM - GEITA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu amesema serikali kupitia mradi wa pamoja imejipanga kunufaisha wanawake, wasichana na wanaume kwa kukuza usawa wa kijinsia pamoja na kuimarisha ustawi wa jamii nchini.
Dkt. Jingu amesema hayo katika kilele Cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya wanawake yaliyofanyika leo Machi 8 2026, Mkoani Geita.
"Mradi wa pamoja una thamani ya shilingi bilioni 262 na unalenga kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa kutoa mikopo ya riba nafuu kwa vikundi vya wanawake na wasichana ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo' amesema Dkt. Jingu..
Aidha, amefafanuwa kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa vituo 200 vya kulelea watoto mchana (Day Care Centres) ambavyo vitawawezesha wanawake kujikita katika shughuli za uzalishaji mali huku watoto wao wakipata malezi bora na salama wakati wa mchana.
"Wizara kupitia mradi wa Pamoja imejipanga kuweka mkazo katika kuwawezesha na kuwashirikisha wanaume kushiriki kikamilifu katika mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia, pamoja na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu madhara ya mila na desturi potofu zinazodumaza maendeleo ya wanawake na wasichana" amesema Dkt.Jingu.
Katika kuimarisha huduma za ulinzi na usalama kwa waathirika wa ukatili, serikali pia itajenga nyumba salama 10 zitakazotumika kuwahifadhi na kuwasaidia waathirika kupata msaada wa haraka, kuboresha mazingira kwa kukarabati ofisi za Maafisa Maendeleo ya jamii naUstawi wa Jamii kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi, pamoja na watajengewa uwezo Wahudumu wa afya ili kuimarisha huduma za afya na ustawi wa jamii kwa makundi mbalimbali.
Dkt. Jingu amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kuongeza usawa wa kijinsia, kupunguza ukatili wa kijinsia na kuinua hali ya uchumi kwa wanawake na familia kwa ujumla na amesisitiza
kuwa ushirikiano wa jamii, taasisi na wadau mbalimbali ni muhimu ili kuhakikisha malengo ya mradi huo yanafikiwa na kuleta maendeleo endelevu nchini.