Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

AHADI SIKU 100 ZA RAIS SAMIA UTOAJI MIKOPO KWA WANACHI YATEKELEZWA MLIMBA

Imewekwa: 19 Dec, 2025
AHADI SIKU 100 ZA RAIS SAMIA UTOAJI MIKOPO KWA WANACHI YATEKELEZWA MLIMBA

AHADI SIKU 100 ZA RAIS SAMIA UTOAJI MIKOPO KWA WANACHI YATEKELEZWA MLIMBA 

📌VIKUNDI VYA WANAWAKE, VIJANA NA WENYE ULEMAVU MLIMBA VYAWEZESHWA

Na Mwandishi Wetu WMJJWM- Morogoro 

Halmashauri ya Wilaya Mlimba mkoani Morogoro imetekeleza ahadi iliyotolewa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutoa mikopo ya thamani ya bilioni 200 kwa vijana na wanawake. 

Akikabidhi hundi za mikopo ya shilingi milioni 466,160,000/= Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju tarehe 18 Desemba, 2025 amesema uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba umetekeleza kwa vitendo ahadi hiyo kwa wananchi.

Amesema mikopo hiyo inayokwenda kwa vikundi 41 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba Morogoro ambapo vikundi vya wanawake (27), vijana(12) na watu wenye ulemavu (2) ambao wamepokea jumla ya pikipiki 21, bajaji 2 iwe chachu ya kuleta mabadiliko katika jamii hasa katika kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo.

"Niwapongeze viongozi kwa kuweka mifumo mizuri ya utoaji na usimamizi wa mikopo kupitia Benki ya NMB kwa kuzingatia Kanuni za Utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambapo imesaidia wilaya kutokuwa na mikopo chechefu." amesema Wakili Mpanju 

Aidha, Wakili Mpanju amekabidhi gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye thamani ya shilingi milioni 207 litakalotumika kwa ajili ya ufuatiliaji mikopo hiyo, kuhamasisha na kusimamia uundwaji wa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu sambamba na uimarishaji wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwenye kata 16 za Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba.

Wakili Mpanju Mpanju ametoa rai kwa wakurugenzi kutoka Halmamshauri zingine kuimarisha Idara za Maendeleo ya Jamii kwa kuwapatia vitendea kazi ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.

Pia Wakili Mpanju amewataka wana Mlimba kudumisha amani, umoja, upendo na mshikamano kwa kuwa ndiyo msingi mkuu wa kuchochea maendeleo ndani ya jamii na kuacha kupotoshwa na watu waliokengeuka na kuwataka vijana na jamii kuepuka mtu yeyote anayetaka kuleta mifarakano katika jamii na kutoa taarifa mara wanapoona vitendo vinavyohatarisha amani.

Naye  Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Dunstan Kiobya amesema kiasi cha shilingi bilioni 2.1 ya mikopo imetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba tangu kufunguliwa upya kwa dirisha la utoaji mikopo ambapo jumla ya vikundi 195 vimenufaika.

Akiongea kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Gibson Mwakoba amesema Mkoa huo unategemea kutoa  Bilioni 5.7 kwa wananchi katika Halmashauri 9  kuelekea siku 100 za  Rais Samia madarakani.

Nao wanavikundi waliopokea mikopo hiyo wameshukuru Serikali kwa kupatiwa mikopo hiyo ambayo itawezesha kupata faida nyingi ambazo zinagusa masuala ya kiuchumi na kijamii ikiwemo kuwezesha vijana kupata ajira  pamoja na kuongeza pato la Halmashari kupitia kodi katika shughuli zao za vikundi.

MWISHO