ABBOTT FUND YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUBORESHA HUDUMA ZA MALEZI NA USTAWI WA WATOTO NCHINI
Na Saidi Saidi WMJJWM
Novemba 5, 2026
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imepokea ujumbe wa Bodi ya Abbott Fund, ukiongozwa na Bi. Melissa D. Brotz, Makamu wa Rais Mwandamizi wa Abbott, Rais wa Abbott Fund na Mjumbe wa Bodi ya Abbott Fund Tanzania, uliofanya ziara katika Kituo cha Taifa cha Malezi ya Watoto Kikombo, jijini Dodoma, kwa lengo la kukagua miundombinu ya kituo hicho na kushiriki katika shughuli mbalimbali, ikiwemo zoezi la upandaji miti.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Miriam Mbaga, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara, Eliakim Maswi, amesema Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na Abbott Fund Tanzania katika kuboresha huduma za malezi, ulinzi na ustawi wa watoto walio katika mazingira hatarishi, ili kuwawezesha kukua katika mazingira salama na kufikia ndoto zao.
Ameeleza kuwa Wizara inaendelea kuandaa Mpango Mkakati na Mpango wa Uendelevu wa Kituo cha Kikombo kwa kipindi cha 2026/27–2030/31, huku akitaja maeneo matano ya kipaumbele katika ushirikiano na Abbott Fund, ambayo ni kuimarisha usalama na ulinzi wa watoto, usafiri salama wa watoto kwenda shule, kuanzisha shule ya awali, kupanua zahanati ili kujumuisha huduma za afya ya uzazi na mtoto pamoja na kuboresha huduma za usafi, na kujenga nyumba za watumishi pamoja na eneo la kuhifadhi vifaa.
Kwa upande wake, Rais wa Abbott Fund na Mjumbe wa Bodi ya Abbott Fund Tanzania, Bi. Melissa D. Brotz, amepongeza Serikali na watumishi wa Kituo cha Kikombo kwa maboresho yaliyofanyika na kujitolea kwao katika kuhakikisha watoto wanapata malezi, upendo, usalama na matumaini ya maisha huku akieleza kuwa Abbott Fund itaendelea kuangalia fursa za kusaidia elimu, malezi na afya ya watoto nchini Tanzania.
Naye Kamishna wa Ustawi wa Jamii Rehema Kombe Ameishukuru Abbott Fund Tanzania kwa mchango wake katika kuboresha miundombinu, kujenga uwezo wa watumishi na programu za kuwaunganisha watoto na familia zao, akisema ushirikiano huo umechangia kuboresha ubora wa huduma na kuweka mazingira rafiki kwa watoto