Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI GWAJIMA AZINDUA KAMPENI YA “BADILIKA, TOKOMEZA UKATILI

Imewekwa: 01 Aug, 2025
WAZIRI GWAJIMA AZINDUA KAMPENI YA “BADILIKA, TOKOMEZA UKATILI

Na WMJJWM – Kigoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua rasmi kampeni ya “Badilika! Tokomeza Ukatili” .

Akizindua Kampeni hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo la Enabel mkoani Kigoma Julai 28, 2025, Waziri Dkt. Gwajima ametoa wito kwa jamii kubadili tabia, mitazamo na mienendo inayochochea ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Amesisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko huku akijiunga mwenyewe kama balozi wa mabadiliko na Kampeni ikilenga kuvuna mabalozi 150,000 katika mkoa huo.

Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeweka msukumo mkubwa katika kutokomeza ukatili kupitia sera madhubuti na mikakati ya kitaifa kama Sera ya Taifa ya Jinsia ya mwaka 2023 na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II).

Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amelipongeza Shirika la Enabel kwa kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya ukatili, pamoja na kuwawezesha wanawake na wasichana kupitia miradi ya maendeleo kama vile mradi wa “Wezesha Binti” unaotekelezwa Kigoma kuwa mfano bora wa namna vijana wa kike wanavyopatiwa elimu, ujuzi na fursa za ajira kwani unaleta matumaini mapya kwa kizazi kijacho.

Naye Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ubelgiji (ENABEL), Koen Goekint, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa na namna ilivyopokea kampeni hiyo huku akihaidi kushirikiana na Tanzania katika juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia, kulinda usawa wa kijamii na kuwezesha wanawake kiuchumi na kijamii.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mhe. Michael Ngayanila, amesema kuwa Mkoa wa Kigoma umeipokea Kampeni hiyo kwa mikono miwili na wapo tayari kushirikiana na Shirika la Enabel pamoja na wananchi kuhakikisha ukatili unatokomezwa.