WAZIRI GWAJIMA AWATAKA WAHITIMU CHUO CHA VETA KIGOMA KUTUMIA ELIMU WALIYOIPATA KUJIAJIRI.

Na WMJJWM – Kigoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka wahitimu wa Chuo cha VETA Kigoma kutumia ujuzi walioupata kujiajiri na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali, ikiwemo mikopo ya wajasiriamali wadogo, ili kujikwamua kiuchumi.
Dkt. Gwajima ametoa wito huo Julai 29, 2025 katika hafla ya kuwatunuku vyeti wahitimu wa Chuo hicho, sambamba na kutembelea karakana za VETA na kujionea mafunzo ya vitendo yakiwemo umahiri wa kujenga madaraja kwa gharama nafuu na ujuzi wa TEHAMA.
Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya elimu ya ufundi na kuhakikisha vijana wanapata stadi bora zitakazowawezesha kushindana kwenye soko la ajira la sasa.
“Ujuzi mlioupata VETA ni silaha ya maisha, utumieni kuanzisha miradi, kujitegemea, na kusaidia wengine kuinuka,” amesema Dkt. Gwajima.
Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amelipongeza Shirika la Maendeleo la Enabel kutoka Ubelgiji kupitia mradi wa "Wezesha Binti", kwa kusaidia vifaa vya elimu, kupambana na ukatili, pamoja na kuwawezesha wanawake na wasichana katika elimu na kupata ajira zenye staha kwenye shule 25 mkoani Kigoma, zikiwemo za VETA.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mgwanwa Nzota, amewahimiza vijana kutumia elimu ya VETA kwa uadilifu ili kuchangia maendeleo ya mkoa na taifa na kusema kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na chuo hicho kuhakikisha vijana wanapata ujuzi stahiki unaokidhi mahitaji ya soko.
Naye Mkuu wa Chuo cha VETA Kigoma, Mhandisi Paul Kimenya, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kipaumbele katika elimu ya ufundi stadi huku akimshukuru Waziri Dkt. Gwajima kwa kuahidi kushughulikia changamoto za Chuo kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa.