Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI GWAJIMA AWATAKA MAAFISA MAENDELEO KUONGEZA KASI YA UTOAJI ELIMU YA FURSA ZA KIUCHUMI KWA WANANCHI

Imewekwa: 14 Jan, 2025
WAZIRI GWAJIMA AWATAKA MAAFISA MAENDELEO KUONGEZA KASI YA UTOAJI ELIMU YA FURSA ZA KIUCHUMI KWA WANANCHI

Na WMJJWM - Tabora

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kuongeza juhudi katika kutoa elimu na kusambaza taarifa kwa jamii kuhusu fursa mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo zinazotolewa na serikali. Wito huo baada ya kubainika  kwa changamoto ya utoaji hafifu wa taarifa kwa wananchi hali inayowafanya kushindwa kufuatilia na kutumia ipasavyo fursa hizo.  

Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo Januari 11, 2025, wakati wa kufunga ziara yake mkoani Tabora, ambapo alizindua Zahanati ya Mbagwa na kukutana na wanawake walio kwenye majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi wilayani Nzega.  

“Napenda kuwapongeza Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuifikia jamii, ikiwemo kuratibu utoaji wa mikopo kwa vikundi mbalimbali. Hata hivyo, ombi langu kwenu ni kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wananchi ili watambue fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali, kama vile namna ya kujisajili kwenye mfumo wa wafanyabiashara wadogo ili kupata vitambulisho vya kidijitali, vitakavyowawezesha kufikia mikopo yenye riba nafuu kupitia Benki ya NMB” amesema Dkt. Gwajima.  

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai amesema kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kutokomeza ukatili wa kijinsia. Amesema juhudi hizo zimekuwa msaada mkubwa hasa kwa watoto wa kike wanaokumbana na changamoto zinazowazuia kuendelea na masomo.  

Aidha, baadhi ya wanachama wa vikundi vya Wanawake vya kujikwamua kiuchumi na ujasiriamali walitoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuwawezesha wanawake kiuchumi.  

Wanachama hao wameeleza kuwa msaada wa Serikali umewaimarisha katika biashara zao na miradi ya ujasiriamali, hatua ambayo imechangia kuboresha maisha yao na kuchochea maendeleo endelevu kwa familia na jamii kwa ujumla.