WAZIRI DKT. GWAJIMA AWASISITIZIA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI ZINAZOTOLEWA NA SERIKALI

Na WMJJWM - TABORA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali, ikiwemo mikopo yenye lengo la kuwawezesha wananchi kuinuka kiuchumi.
Dkt. Gwajima ametoa wito huo Januari 10, 2025, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Nyandekwa, Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Aidha, Dkt. Gwajima amewahimiza wananchi kufuatilia taarifa mbalimbali zinazotolewa na Serikali kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ili waweze kutambua na kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana. Amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara ndogondogo kujisajili kwenye mifumo rasmi ili kupata vitambulisho vya kidijitali, hatua ambayo itawawezesha kufikia mikopo yenye riba nafuu.
“Ndugu wananchi, nimegundua wengi wenu hamfuatilii taarifa zinazotolewa na Serikali na hivyo mnashindwa kupata taarifa sahihi za uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Naomba mjitahidi kufuatilia taarifa hizi, kama mnavyofuatilia habari za michezo, ili mtambue fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na kuzitumia kujikwamua kiuchumi,” amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mhe. Mohamed Mtulyakwaku amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuongeza utoaji wa elimu kwa jamii ili kuwaongezea wananchi uelewa kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya elimu na uwezeshaji wa kiuchumi.
Wananchi wa Kata ya Nyandekwa wameelezea shukrani zao kwa Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum chini ya uongozi wa Waziri Dkt. Gwajima, kwa kuwatembelea na kusikiliza changamoto zao. Wameeleza kuwa ziara hiyo ni ishara ya dhati ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwajali wananchi wake na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.