WAZIRI DKT GWAJIMA AMWAKILISHA SPIKA DKT. TULIA ACKSON, KUFUNGA MASHINDANO YA KUHIFADHI QUR’AN TUKUFU

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amemwakilisha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, kuhitimisha Mashindano ya Qur’an Tukufu ya akina mama watu wazima wa Mkoa wa Dar es salaam iliyofanyika Jijini Dar es Salaam Agosti 11, 2024.
Waziri Dkt. Gwajima amewakumbusha wanawake kuhusu dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwainua kiuchumi hivyo amewataka kujitokeza kupata mikopo isiyo na riba kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa inayotolewa kwa Wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Aidha, amebainisha zoezi linaloendelea la kuwasajili wafanyabiashara ndogondogo ili wapate vitambulisho vya kwa ajili ya mikopo itakayotolewa na Serikali.
Ameipongeza taasisi ya Aisha Sururu (ASF) iliyoandaa mashindano hayo ya kuhifadhi neno la Mungu akisema ni hatua muhimu katika kupambana na mmomonyoko wa maadili unaochangia ukatili wa kijinsia na kwa watoto na kusema Wizara iko tayari kushirikiana.
Akisoma risala ya Taasisi hiyo, Katibu wa ASF, Mwanaid Bakari amebainisha kuwa, Taasisi hiyo yenye umri wa miaka 20 sasa, pamoja na kuendesha mashindano ya kuhifadhisha Qur’an Tukufu, ASF pia inajihusisha na kutoa elimu bora ya malezi, elimu ya kupambana na ukatili wa kijinsia hasa kwa vijana, ambapo amesema mijadala mbalimbali hutolewa kupitia vyombo vya habari vikiwemo redio, televisheni na mitandao ya kijamii.
Amesema, mashindano hayo tangu yaanzishwe yametimiza miaka 15 na kufanikiwa kuunganisha vikundi mbalimbali vya wajane na wenye mahitaji maalum na kutumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayofanya kwenye kuboresha huduma za kijamii nchini hatua zinazosaidia maendeleo na ustawi wa wanawake pamoja na kumpa tuzo ya shukrani kwa Dkt. Tulia Ackson kwa kukubali kuwa mgeni rasmi.
Katika Hafla hiyo, Spika Dkt. Tulia Ackson ameahidi kuchangia shilingi milioni 5 kwa ajili ya kusukuma ujenzi wa majengo ya chuo cha kuhifadhisha usomaji wa Qur’an na Ufundi Stadi kwenye kiwanja kilichopo katika Kijiji cha Kiparang’anda, Wilaya ya Mkuranga.
*MWISHO*