Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MAAFISA MAENDELEO YA JAMII WAASWA KUTUNZA PIKIPIKI.

Imewekwa: 25 Oct, 2025
MAAFISA MAENDELEO YA JAMII WAASWA KUTUNZA PIKIPIKI.

MAAFISA MAENDELEO YA JAMII WAASWA KUTUNZA PIKIPIKI.

 

Na Mwandishi Wetu WMJJWM- Geita

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalum Wakili Amon Mpanju amewaasa Maafisa Maendeleo ya Jamii mkoani Geita waliopatiwa pikipiki ambazo zimetolewa na Serikali ya awamu ya sita  kuzitunza pikipiki hizo na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na sio shughuli zao binafsi.

 

Wakili Mpanju ametoa wito huo tarehe 24 Oktoba 2024 alipokuwa akikabidhi pikipiki nane (8) kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata za Muganza, Kigongo, Lwamgasa, Shabaka, Uyovu, Namonge, Masumbwe na Lulembela katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.

 

Wakili Mpanju ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejikita katika kutekeleza matakwa ya kikatiba ya kugatua rasilimali fedha, ushushaji wa huduma pamoja na watumishi ili kuwafikia wananchi wote walioko katika vitongoji, vijiji, mitaa na Kata na katika hili ndani ya miaka miwili Sekta ya Maendeleo ya Jamii imeajiri watumishi zaidi ya elfu moja.

 

“Serikali imeona kuajiri wataalam wa Maendeleo ya Jamii kwenye Kata pekee bila kuwapatia vitendea kazi inakuwa haitoshi kama tunavyojua jiografia ya Nchi yetu ni pana, kuna baadhi ya wananchi wanaishi mbali na Makao makuu ya Halmashauri. Hivyo Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao ni wachechemzi na wahamasishaji wakubwa wa maendeleo ambao wanatakiwa wahakikishe wananchi wanatambua fursa mbalimbali zinatozolewa na Serikali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu kwa kuwahamasisha katika maeneo yao." amesema Wakili Mpanju

 

Wakili Mpanju ameongeza kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata wana uwezo, mbinu na kuamsha ari ya maendeleo katika ngazi ya msingi kwa kutekeleza majukumu mbalimbali kwa manufaa ya jamii lakini wanahitaji nyenzo za kuwawezesha kuwafikia wananchi hao. Hivyo katika kutambua hilo Serikali imeweka utaratibu wa kununua pikipiki kila mwaka, ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 imenunua pikipiki 98 ili kuboresha utendaji kazi wa Maafisa hao wakishirikiana na wataalam wengine kwenye Kata na kutimiza majukumu yao kiufanisi.

 

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Geita Martha Kaloso ameeleza kuwa Idara ya Maendeleo ya Jamii mkoani humo inakabiliwa na uhaba wa vyombo 131 vya usafiri kwa wataalam wake katika ngazi ya Kata hali inayopelekea uwajibikaji hafifu wa kuwafikia wananchi walioko maeneo ya vijiji vya mbali, ufuatiliaji hafifu wa shughuli za miradi ya maendeleo ya Jamii na ufuatiliaji hafifu wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

 

Nao Maafisa Maendeleo ya Jamii waliopokea pikipiki hizo akiweko Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Namonge Wilaya ya Bukombe Wajama Bwire ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwakumbuka na  kuwapatia pikipiki zitakazowawezesha kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo ambayo yako mbali na makao makuu ya Halmashauri zao.

 

MWISHO