Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI DKT. GWAJIMA AHIMIZA WANAWAKE KUJIUNGA NA MAJUKWAA YA UWEZESHAJI KIUCHUMI

Imewekwa: 13 May, 2025
WAZIRI DKT. GWAJIMA AHIMIZA WANAWAKE KUJIUNGA NA MAJUKWAA YA UWEZESHAJI KIUCHUMI

Na WMJJWM – Dar es Salaam

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewahimiza wanawake nchini kujiunga na vikundi pamoja na majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, ikiwa ni utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza Mei 12, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha wanawake kujiunga na majukwaa hayo, Dkt. Gwajima alisema serikali kupitia Wizara imeunda Kamati ya Hamasa kwa ajili ya kutoa elimu juu ya umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika majukwaa hayo.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha wanawake kupata fursa mbalimbali za kiuchumi zinazowawezesha kujitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa.

Dkt. Gwajima alitoa wito kwa wadau wa maendeleo, taasisi za fedha, sekta binafsi na mashirika ya kiraia kushirikiana na Serikali katika kufanikisha kampeni hiyo kwa pamoja ili kufungua milango ya uwezeshaji kwa wanawake.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. John Jingu, alisema majukwaa hayo ni jukwaa la wanawake kujadiliana changamoto, kujifunza masuala ya biashara, kupata elimu ya kifedha na kutafuta masoko ya bidhaa zao, hivyo kuongeza mchango wao katika uchumi wa familia na taifa.

Mlezi wa Kamati ya Hamasa, Dkt. Judith Mhina, alieleza kuwa lengo ni kuhakikisha kila mwanamke nchini anafikiwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ili asipitwe na fursa za kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Bw. Badru Abdulnuru, alisema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia majukwaa hayo.