Habari

Imewekwa: Aug, 03 2022

WAZIRI DKT. GWAJIMA, AFURAHISHWA MFUMO WA ELIMU MONTASSORI.

News Images

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amefurahishwa na Mfumo wa Elimu unaotolewa na Taasisi ya Montassori huku akizitaka Jumuiya hizo za Montessori kuwafikia watoto wa Hali zote katika jamii ili kuwapatia fursa ya kupata Elimu ya Awali kwani Elimu hiyo ni ya muhimu sana kwa ufahamu wa Mtoto.

Dkt. Gwajima, amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 ya Jamii za Montessori leo Agosti 03, 2022 Jijini Dodoma ambapo ameipongeza Jumuiya hiyo kwa juhudi zao za kuwapatia watoto Elimu ya Awali inayowawezesha watoto kuwa na udadisi , utambuzi binafsi na kujiamini ba kuwaepusha na ukatili wa aina yoyote.

"Ajenda yangu ya kwanza baada ya Sensa ya watu na Makazi ni kufanya harambee ya ujenzi shirikishi wa vituo vya watoto na kuchukua mbinu ya Montessori ili watoto wengi wanufaike hasa wa pembezoni na hata wale wenye mahitaji Maalum" Alisema Dkt. Gwajima."

Akizungumza wakati wa Maadhimisho hayo, Kamishna wa Ustawi wa Jamii Msaidizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Baraka Makona amesema hatua zilizochukuliwa za urahisishaji wa leseni ya kuendesha Vituo vya Malezi itasaidia wadau kuanzisha Vituo vingi vitakavyowezesha kutoa huduma ya Malezi na elimu ya Awali kwa watoto wengi nchini.

"Upatikanaji wa Leseni umerahisishwa na kuwa ndani ya siku tatu hivyo nawasihi mlete maombi ya Leseni za vituo ili viweze kusajiliwa na Watoto wengi waweze kufaidika zaidi" amesema Makona

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Montessori Martha Dello amesema Vitendo vya ukatili vinatokana na malezi duni na kukosekana kwa Malezi imara kwa watoto hivyo Taasisi yao inashirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wanapata sehemu nzuri za kupata Malezi Makuzi na Maendeleo yao ya Awali kwa ustawi wa Watoto na jamii.

"Vitu haviibuki tu tukiwa watu wazima, ni msingi kutoka utotoni, kuna vitendo vingi vya ukatili kwa sababu ule msingi wa kwanza ulikuwa umeharibika,n ndiyo maana pamoja adhabu nyingi bado vinaendelea" alisema Martha.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto (TECDEN) Mwajuma Rwebangira alisisitiza juu ya umuhimu wa Malezi ya Awali kwa watoto kwani ni hatua mhiku katika ukuaji wa Mtoto kwani ndio inamjenga katika kuwa Rai mwema na mwenye uzalendo na taifa lake.

"Tuendeleze Ajenda ya mtoto ya malezi kwani inawajengea watoto uwezo wa kubaini mambo mbalimbali ya msingi katika umri Mdogo hivyo kuwarahisishia maisha" alisema Bi. Mwajuma

Akitoa Salamu za Ofisi ya Rais TAMISEMI Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Amina Mfaki amesema mbinu za Montessori zimekuwa zikitumika katika kuwaeilimisha watoto wa Tanzania kwa miaka 55 hivyo Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kuweka mifumo mizuri ya kuhakikisha watoto kuanzia Elimu ya Awali wanapata Malezi bora hivyo kuwa na Taifa lenye raia wenye kujitambua, kuwajibika na uzalendo kwa Taifa lao.