WATOTO JIFUNZENI MAMBO YANAYOWAJENGA KIMAADILI - NAIBU WAZIRI MWANAIDI
WATOTO JIFUNZENI MAMBO YANAYOWAJENGA KIMAADILI - NAIBU WAZIRI MWANAIDI
Imewekwa: 14 Jan, 2025

Na WMJJWNM - Dar Es Salaam
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwananidi Ali Khamis amewaasa watoto kutumia muda wa masomo vizuri kwa kujifunza yanayowajenga kielimu, kimaadili na kujiepusha na mambo ya kigeni yasiyofaa.
Naibu Waziri Mwananidi amesema hayo Januari 9, 2025 Jijini Dar Es Salaam katika hafla ya utoaji wa vifaa vya shule kwa Watoto wanaoishi na kulelewa katika Makao ya Watoto Tisa yaliyopo Dar Es Salaam na Taasisi ya LALJI Foundation.
Amesema kwamba , Wizara ina dhamana ya kuratibu na kusimamia utoaji wa huduma za msingi kwa watoto wenye mahitaji maalum waliopo kwenye Makao ya Watoto na vituo vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, hivyo ni muhimu jamii na wadau wa Maendeleo kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha watoto wanaolelewa katika maeneo hayo wanapata mahitaji yao stahiki.
"Kila mtoto atenge muda na kushiriki ibada sawa na imani yake, kujifunza neno la Mungu na kuzingatia mahusiano yake kwa mustakabali wa maisha ya sasa na ya baadaye" amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi.
Aidha ameipongeza Taasisi ya LALJI Foundation, ambayo imeshirikiana na Serikali kwa kugusa maisha ya Watoto 400 wanaoishi katika Makao ya Watoto Tisa yaliyopo Jijini Dar es Salaam ambapo wamepewa sare za shule, soksi, viatu na mabegi.