WAKILI MPANJU AVITAKA VYUO VYA MAENDELEO YA JAMII KUFANYA UTAFITI

Na WMJJWM- Mbeya
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amevitaka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Maendeleo ya Jamii Ufundi vilivyo chini ya Wizara kuwekeza katika tafiti na ushauri elekezi kwa kushirikiana na Vyuo Vikuu na Taasisi nyingine zinazofanya utafiti hapa nchini.
Wakili Mpanju ameyasema hayo Agosti 02, 2025 wakati alipotembelea katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii Ruaha-Iringa, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba-Iringa pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole-Mbeya.
Wakili Mpanju amewapongeza watumishi wa Vyuo hivyo kwa jinsi wanavyoendelea kujituma katika kutekeleza majukumu yao na kuvitaka vyuo hivyo kutekeleza maelekezo ya Wizara ya kutanua wigo wa Programu zinazotolewa na Vyuo hivyo ili kukidhi mahitaji ya soko.
"Tuendane na maelekezo ya Serikali ya Kisera na yanayoakisi mitaala ya sasa ya ngazi ya shule za msingi na sekondari inayosisitiza kwenye kuandaa vijana kupata ujuzi, stadi (amali) na weledi wa fani mbalimbali mseto." amesema Wakili Mpanju
Aidha Wakili Mpanju amevitaka Vyuo hivyo kufanya utafiti wa ufuatiliaji (tracer study) kwa nia ya kujua wanafunzi waliohitimu Vyuo hivyo wako wapi na wanafanya nini ikiwa ni moja ya mkakati wa kupima matokeo na mchango wa Vyuo hivyo katika jamii ya kitanzania.
"Muelekeo wa Wizara kwa sasa ni kuboresha Vyuo hivyo kwa kuhakikisha vinapanuka na kupanda hadhi ambapo baadhi ya Vyuo vitakuwa Taasisi huru zinazojitegemea na nyingine kuwa Kampasi ya Taasisi yetu ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ambapo zitatoa elimu za kozi Programu mbalimbali zinazoshabihiana na taaluma ya Maendeleo ya Jamii kuanzia ngazi ya Astashahada mpaka Shahada." amesisitiza Wakili Mpanju
Katika ziara hiyo Wakili Mpanju amekutana na kuzungumza na watumishi wa Vyuo hivyo na kusikiliza mafanikio na changamoto na namna ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.