TAASISI YA MWANAMKE AFYA YAPONGEZWA UTOAJI KIPAUMBELE TIBA KWA WANAWAKE

Na WMJJWM Dar es Salaam
Taasisi ya Mwanamke Afya Sports Promotion imepongezwa kwa jitihada zake katika kuhakikisha Mwanamke anapewa kipaumbele kwenye kupata huduma bora za afya nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis wakati akihitimisha tamasha la michezo la Mwanamke Afya Fun Run and Sports Bonanza Agosti 08, 2024 mkoani Dar Es Salaam lenye lengo la kukusanya fedha zitakazosaidia kupatikana bima za afya 500.
Naibu Waziri Mwanaidi amesema uwepo wa tamasha hili ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi hususani wanawake, kushiriki michezo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha afya zao na kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile msongo wa mawazo, kisukari, shinikizo la damu na uzito uliozidi.
“Napenda kutumia fursa hii kuendelea kumpongeza Bi. Asmini Kihemba, muasisi wa tamasha hili kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Mhe. Dkt. Samiah Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuhakikisha kila matanzania anapata bima ya afya.” Amesema Naibu Waziri Mwanaidi
Aidha Mhe. Mwanaidi amewasihi wazazi na walezi waliohudhuria tamasha hilo, kutumia fursa hiyo kuwa karibu na watoto na familia zao kwa kuhakikisha kila mtoto anapata malezi chanya ili akue na kufikia utimilifu wake.
Naye Mkurungezi Mtendaji wa Mwanamke Afya Sports Promotion na Muasisi wa tamasha hilo Asmin Kihemba amesema tamasha hilo limelenga kukusanya fedha zitakazowezesha kuwakatia bima za afya wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar ikiwa ni jitihada za kuunga mkono Serikali katika utekelzaji wa Bima ya Afya kwa wote.
”Tunakushukuru sana kwa kutuunga mkono Mhe. Naibu Waziri katika tukio letu hili maalum kwa ajili ya kuwasaidia wanawake kupata uhakika wa matibabu yao kwani tunajionea wanawake wamekuwa wakikumbwa na changamoto nyingi za kiafya” ameeleza Asmin.