SERIKALI YAAGIZA KUANZISHWA KWA MADAWATI YA JINSIA KATIKA VYUO VIKUU NA VYUO VYA KATI

Na WMJJWM, Mwanza
Ili kukabiliana na changamoo ya ukatili wa kijinsia Serikali imewaagiza wakuu wa vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati, Tanzania Bara kuhakikisha wanaanzisha madawati ya Jinsia katika vyuo vyao.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu ametoa agizo hilo wakati akifungua mafunzo ya namna Bora ya uanzishaji na uendeshaji wa Dawati ya Jinsia katika Taasisi ya Elimu ya Juu na Elimu ya Kati, mafunzo yaliyofanyika Jijini Mwanza Machi 18, 2025.
Mdemu amesema matarajio ya Serikali ni kuona vyuo vyote hapa nchini vinakuwa na madawati ya Jinsia yenye muitikio mkubwa kwa wanavyuo, wahadhiri, wafanyakazi na watoa huduma waliopo kwenye maeneo ya vyuo.
“Kwa kutambua juhudi hizi za Serikali, naelekeza vyuo vyote ambavyo havijaanzisha madawati haya vifanye hivyo mara moja kwa kutumia rasilimali za ndani na washirikiane na wadau” amesema Mdemu na kuhitimisha kuwa wakuu wa vyuo wahakikishe madawati hayo waliyoyaanzisha yanafanya kazi kwa ufanisi ili yawe endelevu na yenye tija.
Awali, akimkaribisha Mgeni rasmi Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia toka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bi. Rennie Gondwe alisema kuwa Serikali imefanya jitihada nyingi ikiwemo kuhakikisha madawati mbalimbali yanaanzishwa, lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwa na jamii salama.
Lengo la kuanzishwa madawati hayo ni kupunguza na kuzuia kabisa ukatili wa Kijinsia katika taasisi za elimu. Hadi sasa jumla ya madawati 332 tayari ameanzishwa na waratibu wake wamepatiwa elimu huku Wizara ikiendeleza Mkakati wa kuhakikisha jumla a madawati 612 yanaanzishwa katika vyuo vyote vilivyopo Tanzania Bara.
Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ni Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine Prof. Hosea Rwegoshola, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza Bi. Rehema Mkinza, wadau kutoka Taasisi ya kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Wawakilishi kutoka SMAUJATA na wakuu wa vyuo kutoka Shinyanga, Mwanza na Simiyu.