Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

SERIKALI, UNICEF KUIMARISHA USHIRIKIANO WA ULINZI, USALAMA WA WATOTO NCHINI

Imewekwa: 25 May, 2026
SERIKALI, UNICEF KUIMARISHA USHIRIKIANO WA ULINZI, USALAMA WA WATOTO NCHINI

Na Saidi Saidi, WMJJWM – Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amefanya mazungumzo na Mwakilishi wa UNICEF Tanzania, Elke Wisch, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika kulinda haki za watoto, wanawake na makundi maalum pamoja na kuboresha mifumo ya ustawi wa jamii nchini.

Kikao hicho kimefanyika Mei 21, 2026 jijini Dodoma ambapo viongozi hao wamejadili mafanikio yaliyopatikana kupitia ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali ya Tanzania na UNICEF katika sekta ya maendeleo ya mtoto.

Dkt. Gwajima amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sera, sheria na mipango mbalimbali inayolenga kuhakikisha kila mtoto anakua katika mazingira salama yenye malezi bora, huku akisisitiza umuhimu wa malezi ya kifamilia katika kujenga ustawi wa mtoto. Aidha, amesema ushirikiano huo umewezesha kuimarishwa kwa mifumo ya ulinzi wa watoto katika ngazi za jamii na serikali za mitaa pamoja na kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa UNICEF Tanzania, Elke Wisch, amepongeza jitihada za Serikali katika kuimarisha huduma za ustawi wa jamii na kuendeleza kampeni za uhamasishaji kuhusu haki za watoto, huku akiahidi kuwa UNICEF itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kutekeleza programu zinazolenga ustawi na maendeleo ya watoto nchini.

Aidha, viongozi hao wamejadili changamoto zinazoendelea kujitokeza ikiwemo ukatili dhidi ya watoto, mila kandamizi, uhaba wa rasilimali pamoja na hatari zinazotokana na matumizi ya teknolojia na mazingira ya kidijitali na kukubaliana kuendeleza ushirikiano zaidi kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla.

Maeneo yaliyoainishwa kupewa kipaumbele ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa watoto ngazi ya jamii, kupanua huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia, kuimarisha ulinzi wa watoto mtandaoni pamoja na kuwezesha familia kiuchumi.

MWISHO

slot gacor