Habari

Imewekwa: Jan, 03 2024

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA WADAU MWONGOZO WA KUSAIDIA WAHITAJI

News Images

Serikali itaendelea kushirikiana na Wadau ndani ya Jamii kuhakikisha ustawi wa makundi maalum unaimarishwa ili makundi hayo hasa watoto yanufaike zaidi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, ameyasema hayo Januari 02, 2024 wakati akishiriki chakula pamoja na watoto wenye mahitaji maalum katika kituo cha kutunza watoto hao cha Human Dream Children's Village, Wilaya ya Temeke mkoa wa Dar Es Salaam.

Waziri Dkt. Gwajima, ametumia fursa hiyo kuwapongeza Wakuu wa Mikoa kwa kuratibu vema zoezi la kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kushiriki chakula na watoto wenye mahitaji maalum katika kipindi cha sikukuu ya mwaka mpya wa 2024.

Waziri Gwajima amesema, katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka amepokea maoni ya Wadau mbalimbali kuhusu kuimarisha uratibu wa Wadau wanaopenda kusaidia jamii ya makundi maalum ambapo ameona ni jambo jema na ameahidi kuunda Kamati ya Kijamii ili kuratibu wazo hilo ili utengenezwe mwongozo maalum wa uratibu endelevu.

"Hafla hii ya leo pia inatukumbusha kuhusu matunda ya ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi katika kufikisha huduma za kijamii hususan kwa wenye mahitaji maalum hivyo, ni wazo jema kwamba, tuimarishe uratibu wa kijamii." amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Ameongeza kwamba Serikali kwa ushirikiano na wadau wa sekta binafsi inaratibu huduma ya makao ya watoto kwenye vituo 342 vyenye watoto zaidi ya 12000 na vituo vya kulelea watoto wadogo mchana 3,315 vyenye watoto takribani laki 3 hivyo, amewashukuru wote wameendelea kujitoa kuwagusa watoto na makundi mengine.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Elihuruma Mabelya amepokea changamoto zilizoelezwa na kituo hususan miundombinu ya barabara na kuahidi kuingiza mpango wa kuboresha barabara hiyo kupitia mapato ya ndani. Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt Mohamed Mang’ona ameahidi kuongezea wataalamu wa afya kwa ajili ya kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalum.

Kwa upande wake, Kiongozi wa kituo hicho Bi. Nicole Mtawa akiwasilisha risala yake, amebainisha mafanikio katika kuwatunza watoto wenye mahitaji maalum ambapo tangu kianzishwe mwaka 2015, baadhi ya watoto wamepata nafuu na wengine kupona hivyo kujiunga na watoto wengine katika masomo.

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi wa Benki ya TCB, Deo Kwiyukwa, amesema, Benki ya TCB iko tayari kushirikiana na wizara kupeleka elimu kwenye jamii kuhusu huduma za kibenki kwa wanawake na makundi maalumu ili watumie fursa za kibenki ikiwemo huduma za akaunti pasipo makato.

Hafla hiyo iliyodhaminiwa na Benki ya TCB kwa ushirikiano na Taasisi ya CSEMA na AMO foundation, imeratibiwa na taasisi ya FAGDI ambayo ina ushirikiano na wizara katika shughuli za kijamii.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Temeke Mhe. Dorothy Kilave ambaye, alitoa salaam za Mbunge wa Jimbo la Mbagala, Mhe. Chaurembo na kuomba Benki ya TCB ianzishe programu mahsusi kwa ajili ya wanawake wajane.