SERIKALI INATHAMINI MCHANGO WA WATOA HUDUMA YA USTAWI WA JAMII- NAIBU WAZIRI MWANAIDI

Na WMJJWM,Tanga.
Serikali kupitia Wizara za kisekta na Idara ya Ustawi wa Jamii imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa maafisa Ustawi wa Jamii wanafanya kazi katika mazingira bora kwa kutunga Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo inayoakisi mazingira ya Mtanzania.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis katika Kongamano la Kitaifa la Ustawi wa Jamii na Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii nchini (TASWO) Machi 18,2025 Mkoani Tanga.
Mhe. Mwanaidi ameeleza kwamba Serikali inathamini mchango wa Wataalamu wote wa Kisekta hususani Wanataaluma na Watoa Huduma za Ustawi wa Jamii kwani huduma wanazotoa zinagusa moja kwa moja maisha ya watu wa kila aina bila kujali jinsia, dini, itikadi wala kabila.
“Serikali inaendelea kutoa nafasi za ajira kwa Maafisa Ustawi wa Jamii, jambo linaloongeza nguvu kazi na kuboresha huduma kwa jamii lakini pia kutokana na umuhimu wake Serikali iliunda Tume ya Haki Jinai ambayo ilibaini umuhimu wa kuanzisha Idara huru ya Ustawi wa Jamii inayojitegemea kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma katika sekta hii muhimu.” Amesema Mwanaidi.
Aidha, Mhe. Mwanaidi amefafanua kwamba Serikali inakamilisha uundwaji wa Sheria ya Wataalamu wanaotoa Huduma za Ustawi wa Jamii kwani uwepo wa sheria hiyo utarahisisha uratibu na utetezi wa makundi yanayohudumiwa na Wataalamu hao.
“Mnatakiwa Kuimarisha mahusiano katika familia na ndoa kwa kuanzisha programu za kuzijengea familia uwezo, kusimamia na kufuatilia uanzishaji na uendelezaji wa vituo vya kulelea watoto wachanga/wadogo, kuhakikisha kunakuwa na Mikakati ya Kijamii ya malezi bora ili kuzuia watoto kwenda mitaani na kubaki kwenye familia, kuimarisha huduma ya malezi mbadala na kuasili, kusimamia uanzishaji wa nyumba salama kwa ajili ya hifadhi ya waathirika wa ukatili na kuendeleza utoaji wa elimu na uhamasishaji kuhusu utokomezaji wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto”. Amesisitiza Mwanaidi.