NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII SMZ ATEMBELEA MAKAO YA TAIFA YA WATOTO KIKOMBO

Na WMJJWM-Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake Wazee na Watoto kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Khatib Madini Khatib amefanya ziara ya kutembelea Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo pamoja na Kituo cha Kulea na Watoto Mchana cha Giant Fountain Gate yaliyopo Jijini Dodoma Januari 16, 2025.
Lengo la ziara hiyo ni kujionea na kujifunza namna ambavyo vituo hivyo vinatoa huduma za malezi, ujuzi, elimu, afya, na stadi za maisha kwa watoto.
Khatibu amepongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuweka Miongozo na kanuni bora za malezi ya watoto mchana pamoja na wenye mahitaji maalum, ubunifu wa kuendesha miradi ya kiuchumi kama ufugaji wa samaki na kuku, kilimo cha mapapai na nyanya katika Makao ya Watoto Kikombo.
"Tumejifunza mengi, mazuri, tumeona watoto wakiwa na furaha na wametufurahia sana, hii ni dhahiri kwamba wanapata huduma bora kutoka kwa watumishi wa hapa Makao, tunaipongeza Wizara na watumishi kwa moyo wa kujitolea kulea watoto hawa, nasi tumechukua haya kama sehemu ya kuboresha kwa upande wa Zanzibar" amesema Khatibu.
Kwa upande wake Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando amesema moja lengo la kulea Watoto katika Makao ya Taifa ni kuwapa ujuzi kupitia mafunzo mbalimbali ikiwemo ushonaji, kilimo uifugaji, na michezo ili wanapounganishwa na familia na jamii wawe na uwezo wa kujiingizia kipato.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Giant Fountain Gate Lupi James ameishukuru Wizara kwa kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa lengo la kuhakikisha uendeshaji wa kituo unatoa huduma bora kwa watoto.
Ziara hiyo imeongozwa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando Kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Viongozi Kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametembelea Kituo Cha Giant Fountain Gate Day Care kilichopo Kisasa, pamoja na Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Jijini Dodoma.