NAIBU KATIBU MKUU FELISTER AWATAKA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KUTUMIA MITANDAO YA KIJAMII KUFIKISHA ELIMU KWA UMMA.

Na WMJJWM- Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kutumia mitandao ya kijamiiili kufikisha taarifa za kimaendeleo kwa umma kirahisi.
Amesema hayo Mei 9, 2025, jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jinsia na Wanawake yaliyowahusisha Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Naibu Katibu Mkuu Felister amewapongeza maafisa hao kwa juhudi zao katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwataka kutumia ujuzi watakaoupata katika mafunzo hayo kutumia kuelimisha jamii kuanzia ngazi za kaya na mitaa nchini.
“Kazi mnazozifanya zina maslahi mapana sana kwa jamii, nawasihi mtumie mitandao ya kijamii kutoa elimu za programu mbalimbali ambazo zinatekelezwa na Serikali kwa Maendeleo ya Jamii ili ziweze kuwafikia kwa wananchi kwa upana zaidi” amesema Felister.
Akiwasiilisha mada katika mafunzo hayo Mchumi kutoka Wizara ya Maendeleo Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum Alex Shayo amesema uwepo wa Sera hiyo utasababisha kufikiwa kwa usawa wa kijinsia katika nyanja zote za kijamii.
Shayo ameongeza kwamba Sera hiyo mpya itasaidia kuondoa ukatili wa kijinsia, kuimarisha mila na desturi zenye madhara pamoja na kuongeza idadi ya wanawake katika matumizi ya rasilimali zilizopo katika jamii kwa maendeleo yao.