KAMPENI YA AMSHA ARI "CHANGAMKIA FURSA, JENGA LEO NA KESHO YAKO" YAJA
KAMPENI YA AMSHA ARI "CHANGAMKIA FURSA, JENGA LEO NA KESHO YAKO" YAJA
Imewekwa: 03 Aug, 2025

Na WMJJWM- Mbeya
Kampeni ya Amsha Ari inayolenga kutoa elimu ya fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi nchini inatarajiwa kuanza hivi karibu ikiongozwa na Kaulimbiu isemayo Changamkia Fursa, Jenga Leo na Kesho yako”
Hayo yamebainika Agosti 02, 2025 wakati wa Kikao kati ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Uongozi wa Mkoa wa Mbeya kilicholenga kuweka mikakati ya kuwa na Kongamano kubwa mkoani humo kwa ajili ya Wanawake, wasichana na Wafanyabiashara ndogondogo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho cha maandalizi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema kuwa, Kongamano hilo
linalenga kuwafikia na kuwahimiza wanawake, wasichana na wafanyabiashara ndogondogo (wachuuzi wa bidhaa na mazao, dereva pikipiki bajaj, mama lishe/baba lishe, wasusi, wauza mbogamboga) kutambua na kuchangamkia fursa mbalimbali za uwezeshwaji kiuchumi zilizopo kupitia Sekta za Umma na Binafsi.
Akifungua Kikao cha maandalizi Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa ameishukuru Wizara kwa kupeleka makongamano hayo mkoani humo huku akisisitiza wadau wote waliohudhuria zikiwemo Taasisi za fedha, Taasisi za Uhifadhi wa jamii, viongozi wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, viongozi wa wafanyabiashara ndogondogo, bodaboda na bajaj pamoja na wataalam wa Mkoa na Jiji la Mbeya kushirikiana kwa karibu ili kufanikisha makongamano hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Solomon Itunda amesema Mkoa huo upo tayari na mpango kazi wa makongamano hayo umeshaandaliwa kubainisha makundi lengwa ya makongamano hayo huku akihimiza ushirikiano kati ya Wizara, Mkoa, Wilaya na wadau wengine ili kufanikisha Makongamano hayo.
Kongamano la Wanawake na Wafanyabiashara ndogondogo mkoani Mbeya linatarajiwa kufanyika tarehe 15 hadi16, Agosti, 2025 na litahudhuriwa na watu zaidi ya 3,000 ambao wanatarajiwa kupata fursa mbalimbali za uwezeshaji kiuchumi.