Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

JUKUMU LA SERIKALI NI KUBORESHA MAZINGIRA, UTENDAJI KAZI WA NGOs - DKT. MPANGO.*

Imewekwa: 20 Aug, 2025
JUKUMU LA SERIKALI NI KUBORESHA MAZINGIRA, UTENDAJI KAZI WA NGOs - DKT. MPANGO.*

Na WMJJWM-Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Dkt Philip Isidory Mpango amesema Serikali ina jukumu la kuhakikisha kuwa Mashirika Yasiyo Ya Kiserikali (NGOs), yanatekeleza shughuli zake kwa uhuru na kuzingatia malengo, mipango, mikakati na vipaumbele vya kitaifa, sambamba na misingi ya uwazi na uwajibikaji.

Dkt. Mpango ameyasema hayo katika hotuba yake iliyowasilishwa kwa niaba yake na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kwenye kilele cha Kongamano la NGOs 2025, Agosti 13, 2025

Ameeleza kwamba ni ukweli usiopingika kuwa NGOs zimekuwa zikichagiza jitihada za Serikali katika kuwaletea Wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi na afua mbalimbali hususani katika sekta ya afya, kilimo, elimu,maji, mazingira, utawala bora, ulinzi wa jamii,uwezeshaji wa jamii, miundombinu, mifugo na uvuvi pamoja na sekta nyingine mtambuka.

“Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi ni pamoja na kuboreshwa kwa Mwongozo wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya KiserikaliTanzania Bara (2020) na kuja na Toleo la Mwaka 2024, Mfumo wa Kielektroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2020). Vilevile, Ramani ya Kidigitali ya Utambuzi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali(2022/23-2026/27).” Amefafanua Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango pia ameeleza kufarijika na ushirikishwaji wa Baraza kikamilifu katika mchakato wa uanzishwaji wa Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, utoaji wa maoni kuhusu sheria za kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), utoaji wa maoni kuhusu mahitaji ya kikodi ya Sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwenye Tume ya Rais ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Masuala ya Kodi.