JAMII INAHITAJI ELIMU SAHIHI KUONDOA DHANA HASI KUHUSU USAWA WA KIJINSIA - DKT. GWAJIMA

Na WMJJWM - ARUSHA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuhakikisha wanatoa elimu sahihi kuhusu dhana ya maendeleo yenye usawa wa kijinsia.
Waziri Gwajima amesema kuwa jamii ina uelewa hasi kuhusu dhana hiyo hali inayochangia migogoro ya ndoa na kuzorota kwa maelewano ya kifamilia ilihali ajenda hiyo hailengi eneo la ndoa. Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao kazi cha kujenga uelewa kuhusu Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, kilichofanyika Kuanzia tarehe 14 hadi 15 Januari 2025, jijini Arusha, chenye lengo la kuwajengea uwelewa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhusu utekelezaji wa mpango huo.
"Taasisi ya ndoa inayojitegemea na yenye mfumo wake wa kipekee wa uongozi, ambapo mwanaume anapewa nafasi ya kuwa kiongozi wa familia. Hii haimaanishi dhana ya usawa wa kijinsia inapaswa kuchanganywa na masuala ya ndoa. Changamoto zinazoshuhudiwa kwenye ndoa nyingi leo zinachangiwa na uelewa potofu wa dhana ya usawa wa kijinsia," amesema Dkt. Gwajima. Amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutumia fursa ya kikao hicho kuelimisha jamii kuhusu dhana sahihi ya usawa wa kijinsia kwenye maendeleo ya jinsia zote kuhusu kufikia fursa za maendeleo
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Felister Mdemu, amesema kikao kazi hicho kinatarajiwa kutoa matokeo chanya kwa kuwajengea Wakuu wa Mikoa na Wilaya uelewa kuhusu Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama.
Baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya wamempongeza Dkt. Gwajima kwa juhudi zake za kuendelea kuelimisha jamii kuhusu masuala ya jinsia na kushughulikia maoni yao kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa mpango huo wa kitaifa.