Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

FUNGUENI MACHO NA MASIKIO KUZIFAHAMU FURSA ZA KIUCHUMI: DKT JINGU

Imewekwa: 20 Aug, 2025
FUNGUENI MACHO NA MASIKIO KUZIFAHAMU FURSA ZA KIUCHUMI: DKT JINGU

Na WMJJWM- MBEYA

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu ameitaka jamii kufungua macho na masikio kujua mahali ambapo zipo fursa za kiuchumi ambazo zinatolewa na Serikali pamoja na Taasisi za kifedha kwa lengo la kuwawezesha wananchi kukuza na kuendeleza kipato na Maendeleo ya kiuchumi.

Dkt Jingu ameyasema hayo Agosti 16, 2025 wakati akizungumza katika Kongamano la wafanyabiashara ndogondogo Mkoani Mbeya.

Dkt Jingu ameeleza kwamba wafanyabiashara wanatakiwa kupata uelewa na elimu sahihi ya fursa ambazo zimeandaliwa na serikali kwa ajili yao ili waweze kukuza biashara na kuinua vipato vyao.

“Dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wake wanafahamu na kutumia fursa zilizopo kwa kuanzisha na kuendeleza miradi ya kiuchumi inayowawezesha kujiajiri na kuondoa umaskini wa kipato. Wito wangu kwenu ni mfungue macho na msikio kuzitambua fursa hizi na kuchangamkia ili muimarishe biashara zenu na Uchumi kwa Maendeleo ya endelevu” amesema Dkt. Jingu.

Dkt. Jingu ameongeza kwamba, kwa kutumia mikopo yenye masharti nafuu, itawezesha kukuza biashara kuwa kubwa ambapo zitachangia kipato cha Taifa huku akieleza kuwa Serikali inaendelea kuhimiza walengwa wote kutumia nafasi hizo kwa kuwajibika, kuwa wabunifu, na kwa kushirikiana kwa karibu na wadau wa maendeleo ili kujenga uchumi wa viwanda wa kidijitali kwa kuchangamkia fursa, ili kujenga leo na kesho yetu ili bora zaidi.

Miongoni mwa watoa mada katika kongamano hili Meneja wa Hifadhi Scheme kutoka NSSF Rehema Chuma amesema wafanyabiashara ndogondogo wanafursa ya kunufaika na mikopo, pensheni pamoja na kuunganishwa na taasisi za kifedha.

Kongamono hilo la siku mbili linaongozwa na kaulimbiu inayosema changamkia fursa kujenga leo na kesho yako, lina lengo la kukutanisha wanawake na vijana kupata elimu ya fursa zilizopo kupitia Wizara za kisekta na wadau wengine wa maendeleo.

MWISHO