Habari

Imewekwa: May, 10 2023

FAMILIA FUATILIENI WATOTO, SIO MIFUGO PEKEE- WAZIRI DKT. GWAJIMA

News Images

Familia zimekumbushwa kujadili masuala ya maadili ili kujiepusha na changamoto ya mmomonyoko wa maadili inayotajwa kukithiri ndani ya jamii katika siku za hivi karibuni

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito huo Mei 07, 2023, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mayamaya, kata ya Zanka, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Familia hapo Mei 15, 2023.

Amebainisha kwamba kasi ya kuporomoka kwa maadili inachochewa na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo watoto na vijana wamekuwa wakiiga tamaduni na desturi za jamii zingine zinazokinzana na mila na desturi za mtanzania.

"Maadhimisho haya yanawakumbusha wazazi wote wawili na walezi wajibu wao wa msingi katika malezi ya watoto na familia hasa maeneo makuu matatu ya msingi ambayo ni kumjali mtoto kwa mahitaji ya msingi, kumlinda mtoto dhidi ya ukatili na kuzungumza na mtoto mara kwa mara ili kufahamu changamoto zinazomkabili na kufahamu maendeleo yake kwa ujumla" amesema Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima ametaja changamoto za kiuchumi ndani ya familia kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili ambapo wazazi au walezi wamejikuta wakitumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi na kusahau wajibu wao wa kusimamia malezi na makuzi yenye maadili mema kwa watoto.

"Mtoto anaanzishwa kufanyiwa vitendo vya ukatili toka mdogo hadi anakwenda kufundisha na wengine shuleni na mzazi upo, mbona Ng'ombe na mbuzi mnawafuatilia kuliko watoto, Maadili yanatengenezwa kwenye familia, nyumba za ibada, shuleni na vyuoni ili mtoto apite kote akutane na maadili hivyo tumieni muda wenu kuwafatilia watoto " amesema Dkt. Gwajima

Dkt. Gwajima amesema pamoja na jitihada za Serikali kuhimiza maadili mema na upendo ndani ya familia, bado kuna matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto katika familia, shuleni na kwenye jamii ikiwemo ukatili mitandaoni.

"Taarifa ya Hali ya Ukatili wa Watoto Mtandaoni Tanzania kwa mwaka 2021 inasema, asilimia 67 ya watoto na vijana wenye umri kati ya miaka 12 hadi 17 ni watumiaji wakubwa wa vifaa vya kielektroniki ambavyo ni simu, komputa na runinga ambavyo kwa kiasi kikubwa maudhui yake yanakuwa na viashiria vya maadili yasiyofaa"

Akitoa salamu za Wilaya Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Godwin Gondwe amesema wilaya hiyo imeshaanza mikakati ya kukabiliana na suala la mmomonyoko wa maadili kwa kuwaandaa vijana na wameibeba ajenda ya kupinga ukatili kuwa endelevu ambapo mpaka sasa wameshatengeneza klabu za kupinga ukatili katika Shule zote za msingi na sekondari za Wilayani humo

"Tumeshakutana na walimu wakuu wa shule zote, Maafisa elimu kata, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii kuanzia ngazi ya chini mpaka wilaya" amesema Gondwe..

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo uliokwenda sambamba na mashindano ya mpira wa miguu kwa lengo la kutunza mazingira wamesema wazazi wanatakiwa kusimamia watoto wao dhidi ya mazingira hatarishi kwa kuwapa elimu.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Familia Mwaka huu ni "Imarisha Maadili na upendo kwa Familia Imara" na yataadhimishwa kwenye kila mkoa.

MWISHO