Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

DKT. GWAJIMA AZINDUA KITUO CHA KULELEA WATOTO WENYE UHITAJI MAALUM CHA MWANAMWEMA .

Imewekwa: 12 May, 2025
DKT. GWAJIMA AZINDUA KITUO CHA KULELEA WATOTO WENYE UHITAJI MAALUM CHA MWANAMWEMA .

Na WMJJWM - Dar Es Salaam

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amepongeza kwa dhati juhudi zinazofanywa na Mwanamwema Foundation kupitia uzinduzi wa kituo cha kulelea watoto yatima, watoto wenye ulemavu, na wanaoishi katika mazingira magumu, kilichopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Akitoa hotuba kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko (MB), Mei 09, 2025 Dkt. Gwajima amesema kuwa mradi huo ni mfano bora wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau binafsi katika kusaidia makundi yenye uhitaji maalum.

Ameeleza kuwa jitihada hizo zinaendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma katika maendeleo ya taifa.

“Tunapowaona wadau kama Mwanamwema Foundation wakijitokeza kusaidia watoto hawa, tunapata matumaini kuwa jamii yetu bado ina moyo wa huruma, mshikamano na utu niwatie moyo na kuwahamasisha wadau wengine kusaidia jamii katika changamoto mbalimbali,” amesema Dkt. Gwajima.

Aidha Dkt. Gwajima ameoa rai kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wadau wa maendeleo kuiga mfano wa Mwanamwema Foundation kwa kuwekeza kwa watoto kwa mustakabali wa taifa letu."

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mwanamwema Foundation ambaye ndiye Mmiliki wa Taasisi hiyo Mwanamwema Mohammed amemshukuru Waziri Dkt. Gwajima kwa ushirikiano mkubwa alioutoa pamoja na kuzindua Mradi wa jengo la kulelea watoto wenye mahitaji Maalum katika Taasisi hiyo.

Pia Mwanamwema ameomba ushirikiano zaidi kati ya Taasisi hiyo na wadau wengine pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili kuendelea kutatua changamoto za watoto hao.

Pamoja na hayo wadau kutoka Taasisi mbalimbalj wamejitokeza ikiwa ni jitihada za kuunga mkono Taasisi hiyo na kukuza ustawi mzuri wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.